Home Mchanganyiko NHIF itahakikisha inasimamia haki ya wanachama wake

NHIF itahakikisha inasimamia haki ya wanachama wake

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) akizungumza katika semina ya Wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi waandamizi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Iddi Nyundo Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo kulia ni Mkurugenzi wa Uanachama (NHIF), Mbaruku Magawa na kushoto ni Meneja Uhusiano wa (NHIF) Angella Mziray

………………………………………………………………

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka watoa huduma katika vituo vya afya na hospitali nchi nzima walio katika orodha ya mfuko huo kutowanyanyapaa wanachama wake.

Hayo yametokana na kikao kazi kati ya watumishi wa mfuko huo na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika jana ukumbi wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga alisema, anachofahamu vituo vyote vinavyotoa huduma za afya kwa wateja wa mfuko huo wanaelewa taratibu zilizokuwepo na amesisitiza kila mwanachama anayo haki kupata huduma kulingana na aina ya kadi aliyonayo.

“Nilishawahi kupokea malalamiko katika baadhi ya hospitali, lakini baada ya kufuatilia kwa sasa kila kitu kipo sawa. Unajua mfuko wetu una wateja wengi, kama tutaamua kuacha kufanya kazi a hospitali yoyote basi itapoteza watu kwa kiasi kikubwa.

“Ndiyo maana tumeweka wazi kwa yeyote anayeonyesha kunyanyapaliwa au kutendewa kinyume na taratibu za huduma za kiafya atoe taarifa kwetu tutalishughulikia ndani ya muda mfupi,” alisema Konga.

Aidha, Konga alisema lipo tatizo la wizi au ubadhirifu katika baadhi ya watoa huduma. Mifuko mingi ya bima ya afya duniani inalalamikia wizi unaofanywa kati ya wanachama kudanganya watoa huduma kuwema bili kubwa ya matibabu kinyume na bili halisi au watumishi wasio waaminifu wa NHIF kuuibia mfuko.

“Zipo kesi nyingi tunazifuatilia kwenye baadhi ya hospitali. Lakini kwa sasa tunafanya utafiti. Tukishajipanga tutalimaliza hili tatizo.

“Lakini pia lipo tatizo la wanachama kuendelea kuwa na wategemezi waliopitisha umri wa miaka 18. Tunaamini huyo anatakiwa kuwa katika utaratibu mwingine wa uchangiaji. Ndiyo maana tyliamua kupeleka huduma za bima ya afya kwa wanafunzi ambapo wanalipia Sh 50,400 kwa mwaka,” alisema Konga.

Awali akiwasilisha mada kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi wa Uanachama NHIF, Mbaruku Magawa alisema wamekuwa wakikipa fedha nyingi katika vituo vyote vilivyo kwenye utaratibu wao ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma stahiki.

“Mfano kwa mwaka 2018/19 tumelipa jumla ya Sh Bilioni 339.06 kwa vituo vya afya 7,400 nchini. Hapo zikiwemo hospitaki za mikoa, wilaya, Zahanati na Hospitali ya Taifa,” alisema Magawa.

Alibainisha, kwa sasa mfuko huo ulioanzishwa mwaka 2001 kwa Sheria Sura namba 395 umetimiza miaka 18. Ambapo hadi sasa kuna wanachama 16,969,943 sawa na asilimia 32 ya watanzania wote.

Wanajipanga kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanajiunga na mfuko huo ili kupata huduma za afya kwa wakati na gharama nafuu. Hasa ikizingatiwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaongezeka siku hadi siku.

Akitolea mfano, takwimu za mfuko zinaonyesha mwaka 2014/15 idadi ya wagonjwa waliotibiwa magonjwq yasiyo ya kuambukizwa walikua 286,806.

Lakini ndani ya miaka minne idadi imeongezeka maradufu ambapi takwimu za mwaka 2017/18 zinaonyesha kuna wagonjwa 1,574,803 waliotibiwa kupitia NHIF wakisumbuliwa na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

NHIF imeahidi kuwa karibu na wanachama wake kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kupitia vyombo vya habari ikiwemo elimu juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya lakini pia kuzisaidia baadhi ya hospitali zisizo na uwezo wa kuwa na vifaa tiba kwa kuwapa mikopo ili wanachama wao wapate huduma popote ndani ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) akifafanua jambo katika semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Iddi Nyundo Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo

Mbarouk Magawa Meneja wa Wanachama (NHIF) akiwasilisha mada katika semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Iddi Nyundo Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo

Baadhi ya waandishi wakichangia masuala mbalimbali katika majadiliano wakati wa semina hiyo.

Baadhi ya maofisa wa NHIF wakifuatilia mjadala katika semina hiyo.

Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika semina hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) akiwa katika picha ya pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na baadhi ya waandishi pamoja na maofisa wa NHIF mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo.