Home Mchanganyiko Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yawapiga msasa watumishi wapya

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yawapiga msasa watumishi wapya

0

****************************

Na Dennis Buyekwa
Katika kuhakikisha inatoa huduma bora na yenye viwango, Ofisi ya Wakili Mkuu
wa Serikali kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma imeendesha
mafunzo elekezi kwa watumishi wapya kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine,
yamewahusisha watumishi wapya ambao ni Mawakili, Afisa Kumbukumbu, Afisa
Tehama pamoja na Afisa Habari.

Akizungumzia mafunzo hayo Mkurugenzi wa Utawala na Rasirimali Watu Bw.
James Kibamba, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yamelenga
kuwajengea uwezo wa kimaadili watumishi wapya ili waweze kufanya kazi zao
kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Utumishi wa Umma.

“Mafunzo haya ni muhimu sana hasa kwa Watumishi wapya katika utumishi
wa Umma kwa kuwa yanawasaidia kujua taratibu zote za kiutumishi ndani
ya Utumishi wa Umma”. Alisema Bw. Kibamba.

Aidha Bw. Kibamba amewaasa watumishi hao kufanya kazi kwa bidii pamoja na
kuzingatia masuala ya kinidhamu katika nyanja zote sambasamba na kuwaheshimu watumishi wengine ili kuweza kudumisha mshikamano na ushirikiano uliopo baina ya watumishi wengine wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine Wakili wa Serikali Bw. Samwel Lukelo amewataka
watumishi hao wapya kufanya kazi kwa jitihada ikiwa ni pamoja na kujiepusha na
tabia za kufanya kazi mtu mmoja mmoja na badala yake wafanye kazi kwa
ushirikiano jambo litakalo wasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi Zaidi.

“Nawaombeni mjenge tabia ya kufanya kazi kwa timu, mjiepushe na tabia za
kujifungia na pale mtakapokuta kuna jambo hamlijui msisite kuuliza”
alisema Bw. Lukelo”.

Bw. Lukelo pia amewaasa watumishi hao kujiepusha na tabia ya kufanya kazi kwa
mazoea kwani itawapelekea kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo na
kuwapunguzia ufanisi katika kazi zao. Amewaasa watumishi hao pia kufanya
maandalizi ya kutosha kabla ya kwenda kutekeleza majukumu yao hali itakayo
wasadia kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

Akizungumzia suala la muda Wakili huyo amesema ni muhimu kwa mtumishi
yeyote kutunza na kutumia muda wake vizuri, kwani matumizi sahihi ya wakati
yanamsaidia mtumishi kufanya mambo yake kwa wakati na kwa mpangilio
unaotakiwa.

Aidha amewataka waajiriwa hao wapya kujenga tabia ya kujisomea mambo
mbalimbali ili iwasadie kujiongezea maarifa katika mambo yanayohusiana na kada
zao ili iwasaidie kujua mambo mengi kwa wakati mmoja na hivyo kurahisisha
suala la utendaji kazi miongoni mwa watumishi hao.

Vilevile Bw. Lukelo pia amewaasa watumishi hao kujenga tabia ya kuweka
kumbukumbu ya kazi zao ili itakapotokea hawapo iwe rahisi kwa watumishi
wengine watakaokasimu madaraka yao kuweza kutekeleza majukumu yao kama
kawaida.
Wakizungumza namna walivyoyapokea mafunzo hayo, watumishi hao
wameishukuru Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuamua kuwapatia mafunzo
na kusema yatawasadia kuwajengea uwezo ikiwa ni pamoja na kuwafanya
wajiamini watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Afisa Kumbukumbu wa
Taasisi hiyo Bw. Athuman Zunda aliishukuru taasisi hiyo kwa mafunzo hayo na
kusema wamejifunza mambo mengi yanayohusiana na Utumishi wa Umma
yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria na
taratibu za utumishi wa umma.

Sambamba na mafunzo hayo watumishi hao pia walikula kiapo cha Maadili ya
Utumishi wa Umma, kiapo hicho kiliongozwa na Hakimu Mkazi wa mkoa wa
Morogoro Mhe. Juma Ally Mbonde.

Baada ya kiapo hicho Mhe. Hakimu Mkazi aliwataka watumishi hao kufanya kazi
kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matukio yaliyo kinyume na
Utumishi wa Umma hasa yale yanayohusiana na vitendo vya rushwa.