Hadi kufikia Machi mwaka huu, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 432,285,137 sawa na asilimia 117.06 ikiwa imevuka lengo katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Katika mwaka huo wa fedha, Taasisi hiyo ilikadiriwa kukusanya shilingi 371,000,000 kutoka vyanzo vyake vya tozo za ramani na machapisho ya jiosayansi, tozo za huduma ya maabara na ada za ushauri elekezi kwa mwaka wa fedha.
Hayo yalisemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Madini Doto alipokuwa akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2019/20.
Waziri Biteko alisema kuwa mafanikio hayo ya GST yametokana na jukumu kubwa la kufanya tafiti za jiosayansi kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini.
“Kupitia tafiti hizi taarifa mbalimbali za jiolojia na uwepo wa madini nchini zinaandaliwa kwa lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa migodi mipya. GST ilikamilisha ugani wa jiolojia na jiokemia katika QSD 202 iliyopo Kibaha mkoani Pwani na QSD 49 iliyopo katika wilaya ya Maswa”
Aidha, Waziri Biteko aliongeza kuwa GST kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia ya China ilikamilisha utafiti wa jikemia kwa skeli kubwa katika mkoa wa Mbeya na skeli ndogo nchi nzima.
Ambapo, katika kipindi kinachoishia Machi 31 mwaka huu, GST ilifanya uchunguzi wa madini katika sampuli 10,740 ikilinganishwa na lengo la sampuli 7,500 iliyojipangia.
Waziri Biteko alisema kuwa uchunguzi huu ulilenga kubaini uwepo, ubora, na kiasi cha madini katika sampuli hizo.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa GST inaendelea kutoa huduma zake za maabara zinazokidhi viwango vya kimataifa, maboresho ya mifumo ya uendeshaji wa huduma zake yalifanyika na kukaguliwa na Taasisi ya inayosimamia ubora wa huduma zinazotolewa na maabara duniani kote (SADCAS).