Polisi Mkoani Mbeya inawashikilia watu wanne [04] kwa kosa la mauaji. Mnamo tarehe 17.05.2019 saa 21:45 usiku huko katika Kijiji cha Isangala, Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa makusudi na bila halali watuhumiwa walimuua TENSON NDEGE META [54] kwa kumshambulia na vitu butu na vyenye ncha kali na kisha kumweka kwenye buti ya Gari na kwenda kumzika huko Wilayani Chunya.
Watuhumiwa waliofanya tukio hilo ni:-
DEVI SIMBAZYE @ MKOMBE [44] Mganga wa kienyeji na mkazi wa Isangala – Mbeya Vijijini.
PETER SIMON NDEGE [43] Mkazi wa Kibaoni – Chunya.
ALLY SHAIBU MTUKWA @ KAMGUU [51] Mkazi wa Itewe – Chunya.
LAMECK LEONARD MWANYANJE [39] Mkazi wa Majengo – Chunya.
Baada ya mauaji hayo mwili wa marehemu ulizikwa bila kufanyiwa uchunguzi. Polisi tumeomba amri ya Mahakama ili kufukua mwili huo na kuufanyia uchunguzi na juhudi za kuwasaka watuhumiwa wengine waliotoroka zinaendelea.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaosababisha vifo vya wenzao, pia tunataka waganga wa jadi kuacha mara moja kupiga ramli chonganishi. Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa rai kwa wana Mbeya wote kujiepusha na imani potofu za kuamini sana masuala ya ramli na kutofika Mahospitalini pale wanapougua.
Wakati huo huo Polisi Mkoani Mbeya inamtafuta Dereva wa Gari la kusafirisha vipodozi na pombe haramu toka Zambia ambaye amesababisha ajali na kumgonga dereva wa Pikipiki @ Bodaboda na kusababisha kifo chake mnamo tarehe 25.05.2019 saa 02:50 usiku huko katika barabara kuu ya Mbeya kuelekea Mkoa wa Songwe, maeneo ya Tarafani, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, ambapo tulikamata gari yenye namba ya usajili T.860 BHD aina ya Mark II Bliz na wakati wanakimbia waligonga pikipiki yenye namba ya usajili
T.249 BPF aina ya T-Better na kusababisha kifo cha Dereva wa pikipiki hiyo aitwaye EMMANUEL SAMUEL KAJANGE [37].
Katika msako huo tumekamata Pombe haramu na vipodozi vya aina mbalimbali kama ifuatavyo:-
Maboksi ishirini [20] ya vipodozi vya aina mbalimbali,
- Maboksi ishirini na nne [24] ya pombe aina ya “White Spirit”
- Chupa ishirini na moja [21] za mafuta ya kupaka aina ya dodo kutoka nchi jirani ya Zambia bila vibali.
Aidha tunawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni:-
FLORA RUBEN [48] Mkazi wa Uyole Jijini Mbeya
- MAWAZO MASAU [31] Mkazi wa Sokomatola Jijini Mbeya kwa kuagiza na kufanya biashara hiyo ya magendo.