Home Mchanganyiko BABU WA LOLIONDO AUNGANISHWA NA UMEME WA REA

BABU WA LOLIONDO AUNGANISHWA NA UMEME WA REA

0

Na Ahmed Mahmoud Ngorongoro

MCHUNGAJI mstaafu wa kanisa la KKKT, ambae kwa sasa anatoa huduma ya matibabu ,Ambilikile Mwaisapile, ameipongeza serikali kwa kuwasha umeme nyumbani kwake na kusema kuwa sasa amepata mwanga atafanya kazi zake  hata nyakati za usiku tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kupata umeme.

Mchungaji  Mwaisapile maarufu babu Kikombe wa Samunge, wilayani Ngorongoro,ameyasema hayo jana nyumbani kwake mara baada ya waziri wa Nishati Dakta Medadi Kalemani, kuwasha umeme wa REA nyumbani kwake.

 Mwaisapile, amesema hakutegemea kama kuna siku angelipata Umeme lakini sasa ameishukuru serikali kwa kumuwashia umeme wa Rea, nyumbani kwake.

Amesema kutokana na serikali kutekeleza miradi ya umeme Vijiji Tanzania itakuwa ni kioo cha maendeleo barani Afrika.

Akizindua na kuwasha umeme huo Waziri wa Nishati,Dakta Kalemani, amesema serikali ipo katika kutekleza miradi ya umeme vijijini kupitia REA,na kurejea maelekezo yake kwa wakandarasi kuhakikisha hakuna Kitongoji ,Kijiji,Kata ambayo nyumba haitapata umeme hata kama ipo chini ya miti lazima ipatiwe umeme.

Amesema Mwaisapile ameitangaza Samunge na Tanzania Ulimwenguni kutokana na tiba yake kwa watu mbalimbali ambao huwa wanafika nyumbani kwake kupnywa kikombe cha dawa.

Amesema mradi huo wa umeme wa REA ulofungwa nyumbani kwa Mwaisapile,unatokea kijiji cha Wasso,wilayani Ngorongoro umbali wa kilometa 335 .

Amewahakikishia wananchi wilayani Ngorongoro kuwa kila  mmoja atapata umeme nyumbani kwake kabla ya Desema 30 mwakani.

Ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkandarasi wa umeme wa REA kampuni ya Nipoco, kuhakikisha Vijiji na Vitongoji vyote wilayani humo vinapata umeme huo wa REA bila kusahau au kuacha au kuruka nyumba hata moja.

 Ameongeza kuwa mwisho wa wakandarasi nchini kusambaza umeme Vijijini nchini kote ni Desemba 31 mwaka huu kulingana na mikataba yao hivyo lazima waongeze kasi ya usambazaji umeme.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Ngorongoro Willium ole Nasha, ameipongeza serikali kwa mafankio hayo ya kusambaza umeme vijijini katika kipindi cha miaka mitatu na kuiwezesha wilaya hiyo katika kipindi hicho kuwa na maendeleo makubwa  .

Nasha,ambae pia ni Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,amesema kutokana na kupatikana kwa umeme tayari serikali imeshatoa shilingi milioni 800 kwa ajili  ya ujenzi wa chuo cha ufundi VETA, na kitaanza rasmi Augosti mwaka huu .