Home Mchanganyiko WANAKIJIJI CHIKONGO WASHUPALIA MAPATO NA MATUMIZI

WANAKIJIJI CHIKONGO WASHUPALIA MAPATO NA MATUMIZI

0

Na Mwandishi wetu Mihambwe

Kamati ndogo ya kuchunguza mapato na matumizi imeundwa katika mkutano wa hadhara wa kijiji cha Chikongo baada ya Wananchi kuchachamaaa kwa kuikataa taarifa ya Serikali ya kijiji.

Sakata hilo limeibuka kwenye mkutano wa robo ya tatu ya mwaka katika Kijiji cha Chikongo kilichopo kata ya Mkoreha mbele ya Afisa Tarafa ya Mihambwe Gavana Emmanuel  Shilatu baada ya  Wananchi kutokuwa na imani na ripoti iliyosomwa kutowaridhisha .

Kutokana na tafran hiyo  Afisa Tarafa ya Mihambwe Emmanuel Shilatu aliagiza mara moja  iundwe  kamati ndogo itakayopitia mapato na matumizi ya Kijiji hicho jambo ambalo  liliungwa mkono na Wananchi.

Gavana huyo alitaka kamati hiyo ihusishe viongozi wa kata,  Serikali ya Kijiji, baadhi ya Wananchi na wajumbe wa kamati ya ujenzi ili kumaliza utata huo na ukweli ujulikane

“Yapo  madai ya mkutano mkuu wa kijiji hauitishwi kwa mujibu wa kalenda, Wananchi hawasomewi mapato na matumizi, Madai hayo ni ukiukaji  wa sheria. Napendekeza iundwe kamati hapa hapa. Ipekue hesabu kisha ije na majibu ya kuridhisha”  Alisema Gavana Shilatu.

Katika hatua nyingine Gavana Shilatu kupitia mkutano huo aliwataka  Wakulima kuendelea na kazi zao za kilimo na  wajasiliamali kuendelea kupatiwa vitambulisho vya shughuli  zao.

“Mkulima ahakikishe analima, Mjasiriamali apatiwe   kitambulisho. Tunahitaji kila Mwananchi awe mlinzi wa amani. Wote tukifanya kazi ndipo tutakapoinua uchumi wa nchi.” alieleza Gavana Shilatu.

Katika mkutano huo wa Kijiji ulihudhuliwa na Afisa Tarafa Mihambwe, Diwani kata ya Mkoreha, Mtendaji kata na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Chikongo.