Home Mchanganyiko SERIKALI KUWAKAMATA NA KUWAONDOA WALIOVAMIA KIA

SERIKALI KUWAKAMATA NA KUWAONDOA WALIOVAMIA KIA

0

Na Ahmed Mahmoud,Arusha

Serikali imesema kuwa ipo katika hatua za mwisho kukamilisha kuwaondoa wananchi wote waliovamia katika kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (KIA) ili kupisha  shughuli za uendeshaji na maboresho ya kiwanja hicho .

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano,Dkt.Isack Kamwelwe ameyasema hayo mapema  leo jijini Arusha, wakati alipokuwa kwenye mkutano wa tatu wa baraza la wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro, (Kadco) , unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa AICC,jijini hapa.

Waziri Kamwelwe amesema kuwa  suala la uvamizi wa Viwanja vya ndege nchini linalofanywa na wananchi hususani katika kiwanja cha ndege cha KIA,linapaswa kushughulikiwa kwa umakini ili wananchi waweze kupisha eneo hilo na kupatiwa eneo nyingine kwa maendeleo  mapana ya uchumi wa taifa.

“Uwanja wa ndege wa Kia ni moja ya viwanja vya kimkakati nchini katika kuendeleza shughuli za kiutalii ili kukuza uchumi wa taifa” Alisema Waziri

Katika hatua nyingine Kamwelwe alisema serikali imekipa hadhi kiwanja cha KIA kujengwa chuo cha mafunzo  kwa waongozaji wa ndege (Payrot )ili kuwapa fursa ya kupata mafunzo na kuongeza idadi ya waongozaji wa ndege ambao kwa sasa idadi yabwazawa ni asilimia 40 pekee .

Awali Mkurugenzi wa Kadco,Mhandisi  Christopher Mukoma,Alisema Kiwanja cha ndege cha KIA kimepiga hatua kubwa kwa kuongeza  mtaji kutoka  sh,milioni 700 mwaka 1999 hadi kufikia mtaji wa bilioni 31 mwaka huu 2019.

Aidha Alisema kuwa idadi ya abiria wameongezeka kutoka  2000 mwaka 2000 hadi kufikia abiria 850,000 mwaka 2019,hata hivyo Alisema kiwanja hicho kilijengwa na uwezo wa kupokea abiria 500,000 lakini kutokana na maboresho yaliyofanyika hadi sasa kinapokea abiria 1,200,000.

Amesema mafanikio hayo yamewezesha kiwanja hicho kupata faida ya sh bilioni 4 mwaka 2018 na shilingi bilioni 5 kwa mwaka huu na kufanikiwa kutoa gawio la sh,milioni 700 serikalini mwaka Jana 2018.

Mhandisi  Mukoma alisema kuwa  changamoto kubwa inayokikabili kiwanja hicho ni jambo la uvamizi wa wananchi ambao wamekuwa wakipitisha mifugo yao na kupelekea uharibifu mubwa wa mazingira .