Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Felister Shuli (katikati aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (Kazi SACCOS) kilichofanyika Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wakisikiza kwa makini maelezo ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Felister Shuli (hayupo pichani) ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa ofisi hiyo.
Mrajis wa Mkoa wa Dodoma Bw. Revocatus Nyagiro akitoa salamu wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtaa wa Reli, Novemba 28, 2020.
Mwenyekiti wa Kazi SACCOS Bw. Omar Sama (kulia) akitoa maelezo kuhusu chama kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Felister Shuli (katikati). Kulia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo wa saba wa Kazi SACCOS Bi. Vinerose Mtenga.
Mwenyekiti wa Mkutano huo wa saba wa Kazi SACCOS Bi. Vinerose Mtenga akieleza jambo wakati wa mkutano huo. Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Felister Shuli.
Mkaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Bi. Dorah Meta (aliyesimama) akitoa taarifa ya ukaguzi wa Kazi SACCOS kwa kipindi cha Januari – Disemba 2020.
Sehemu ya wanachama wa Kazi SACCOS wakifuatilia kwa makini taarifa ya ukaguzi wa chama hicho.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Felister Shuli (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachama wa Kazi SACCOS, Wajumbe kutoka Saccos ya Chuo Kikuu cha UDOM na Wakaguzi kutoka COASCO.
Mwenyekiti wa Kazi SACCOS Bw. Omar Sama (kushoto) akitoa taarifa kwa wanachama kuhusu eneo linalomilikiwa na chama hicho cha ushirika ambalo linaukubwa wa mita mrada zaidi ya 4,000.
……………………………………………………………………………….
Na; Mwandishi Wetu, Dodoma
Chama cha Ushirika, Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu (Kazi SACCOS) kimefanya mkutano wake mkuu wa tano wa mwaka 2020 Mkoani Dodoma.
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtaa wa Reli, Novemba 28, 2020.
Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Felister Shuli ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu alieleza kuwa vyama vya ushirika ni njia pekee ya kumkomboa mwanachama ili awaze kupata huduma za kimsingi, hivyo muunganiko huo ambao huwakutanisha watu mbalimbali unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha ushirika huo pamoja na wanachama wanatimiza malengo yao kwa pamoja.
“Familia yenye furaha inaanza katika muunganiko huu ambao unalenga kuwezesha wanachama kujiinua kiuchumi wa wenyewe na jamii inayowazunguka,” alieleza Shuli
Aliongeza kuwa, wanachama wanufaika kupatiwa mafunzo ya ushirika, ujasiriamali na stadi za biashara ili waweze kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuinua mtaji wa ushirika wa Kazi SACCOS.
Aidha, Mkurugenzi huyo alipongeza uongozi wa Kazi SACCOS pamoja na wanachama kwa kuona umuhimu wa kuvialika vyama vingine kwenye mkutano huo ili waweze kujifunza namna vyama vingine vya ushirika vinavyotekeleza majukumu yao.
Akiongea katika Mkutano huo Mrajis wa Mkoa wa Dodoma Bw. Revocatus Nyagiro aliwaasa viongozi wa Kazi SACCOS pamoja na Saccos zote nchini kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni na pia kuheshimu na kusikiliza wanachama wa vyama hivyo vya ushirika.
Alieleza kuwa, mwelekeo wa Serikali ni kuimarisha vyama vya ushirika kwa muktadha huo wanachama inabidi watambue wanaanzisha vipi bidhaa mpya ambazo zitahamasisha wanachama kwa kuzingatia ushindani uliopo sasa katika sekta ya fedha.
Sambamba na hayo, amewahimiza viongozi na wanachama wa Kazi SACCOS kuendelea kufanya mikutano mikuu mara kwa mara ili kuimarisha chama hicho.
Awali akitoa taarifa ya Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mwenyekiti wa Kazi SACCOS Bw. Omar Sama amesema kuwa lengo la mkutano huo ilikuwa kutoa taarifa kwa wanachama kuhusu shughuli mbalimbali za chama pamoja na kuweka makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha ujao na mipango ya utekelezaji.
Mara baada ya mkutano huo viongozi wa Kazi SACCOS pamoja na wanachama walitembelea eneo ambalo linamilikiwa na chama hiko cha ushirika lililopo Mtumba, Jijini Dodoma na wanachama hao walipata fursa ya kujionea viwanja vinne (4) ambavyo vinaukubwa wa mita mrada zaidi ya 4,000.