Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kufanya usafi wa
mazingira kwenye Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa Akili ya
Mirembe, iliyopo mkoani Dodoma jana.
*********
Na Mwandishi Wetu, MOHA
UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa Akili ya
Mirembe, mkoani Dodoma, umefurahishwa na kitendo cha
watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda
kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapo.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mganda Mkuu wa hospitali
hiyo, Dkt. Escor Tweve.
Watumishi hao wakiwa na baadhi ya viongozi wa Wizara, idara
zilizopo chini ya Wizara hiyo, waliadhimisha Wiki ya Utumishi
wa Umma kwa kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapo.
“Nawashukuru kwa uamuzi wa kuja kufanya usafi wa mazingira
hospitalini hapa kwa kufyeka, kulima, kuchoma taka, kudeki na
kufanya kazi nyingine za kijamii.
“Mmeonyesha upendo mkubwa mlionao dhidi yetu, mmejitoa
kwa moyo wa dhati, miaka mingi imepita hatujawahi kupata
ugeni uliofanya jambo muhimu kama hili,” alisema Dkt. Tweve.
Mbali ya kufanya usafi wa mazingira, watumishi hao walipata
fursa ya kupewa elimu juu ya huduma zinazotolewa kwa
wagonjwa hospitalini hapo.
Dkt. Tweve alisema changamoto kubwa waliyonayo wagonjwa
wa akili huwa hawapendwi katika jamii ila ni watu wanaopaswa
kupewa upendo mkubwa na jamii.
“Wagonjwa wa akili hawana tofauti na watu wengine ambao
hawana matatizo kama yao kwenye jamii, wanapoletwa hapa
hospitali huwa tunawapatia matibabu, kupona, kutoa michango
mizuri kwenye jamii na nchi kwa ujumla,” alisema.
Aliishukuru Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa
kwani kuna wagonjwa wengine wa akili hukamatwa, kuhitajika
kufanyiwa matibabu hospitalini hapo.
Pia wapo baadhi ya watumishi wa idara za serikali wakiwemo
askari ambao hospitali hiyo huwapatia matibabu ya akili,
kupona, kuendelea na majukumu yao ya kazi.
“Naishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuadhimisha
siku hii kwa kuja Mirembe na kufanya usafi wa mazingira,
nawaomba muwe na utaratibu wa kuja mara kwa mara,”
alisisitiza.
Aliwapongeza watumishi wa Wizara hiyo na viongozi wao
akiwemo Waziri Kangi Lugola, Naibu Waziri, Mhandisi Hamad
Masauni, Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu, Naibu Karibu
Mkuu, Ramadhani kailima kwa utendaji mzuri wa kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAWA katika
Wizara hiyo, Jane Massawe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu,
aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa ushirikiano
walioutoa kwa watumishi hao.
“Tumefurahishwa na mapokezi mliyotupa, tupatapo nafasi kwa
siku nyingine tutakuja kuwatembelea na kufanya shughuli za
kijamii,” alisema Massawe.
Wiki ya Utumishi wa umma ilianza huadhimishwa kuanzia Juni
17 hadi 22, mwaka huu. Maadhimisho hayo ni kwa mujibu wa
Kalenda ya Umoja wa Afrika (AU).
Nchi mbalimbali huadhimisha siku hiyo kwa kushiriki shughuli
mbalimbali zinazohusu utumishi wa umma.