Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe. Ainawe Moshi , akizungumzia maboresho ya mahakama hiyo.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe
********************************
Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Bukombe
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe. Ainawe Moshi amesema kwamba Mahakama za Mwanzo katika Mkoa wa Geita zimejipanga kumaliza mashauri ndani ya kipindi cha miezi minne, licha ya utaratibu uliopangwa wa miezi sita.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Mahakama ya Tanzania, jana (8.06.20) kwenye ofisi ya Mahakama hiyo, wilayani Bukombe, Hakimu huyo alisema mahakama hizo zimejipangia utaratibu huo licha ya kuwepo kwa muda maalumu wa kusikiliza shauri, ili kuwawezesha wananchi kupata fursa ya kutosha ya kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
‘‘Napenda kuwaambia wananchi na wadau wetu kuwa Mahakama ya Tanzania imeboresha miundombinu, hivyo sisi tumejipanga kumaliza mashauri kwa wakati tofauti na zamani ambapo watu walikuwa wanafahamu shauri linaweza kukaa miaka miwili hadi saba mahakamani . Lakini kwa sasa hivi Mahakama inaenda na wakati hakuna shauri la Mahakama ya Wilaya linalokaa zaidi ya miezi 12, pia kwa Mahakama za Mwanzo tumejipanga kumaliza shauri ndani ya miezi minne,’’ alisema Moshi.
Aliongeza kuwa wananchi wasiogope kufikisha mashauri yao mahakamani, bali wafike kwenye eneo hilo na watapata haki zao bila upendeleo kwa wakati.
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya, Bukombe, Bw.Sauwael Urio alisema kutokana na maboresho yaliyofanyika hivi sasa wanatoa nakala za hukumu ndani ya siku 21. Hivyo hali hiyo imetokana kuwepo kwa mazingira wezeshi ya vitendea kazi na watumishi wa kutosha.
Alisema mahakama hiyo inapokea wastani wa mashauri 600 kwa mwaka na kuhudumia takribani wananchi 200,000 wanaotoka kwenye wilaya hiyo na Wilaya ya Mbogwe.
Aliongeza uwajibikaji na hamasa ya utendaji kazi imeongezeka kwa kuwa hakuna tatizo la baadhi ya watumishi kukosa nafasi ya kufanya kazi na vitendea kazi hivi sasa halipo.
Naye Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushirombo, Mhe. Damas Gakwaya alisema wanafanikiwa kusikiliza mashauri ngazi za mahakama hiyo kwa kipindi cha miezi miezi minne kwa sababu wanayapokea tayari yakiwa na shahidi uliokamilika. Pia hutumia utaratibu wa kuwa karibu na wananchi ili kuwasaidia kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria . Mahakama hiyo kwa mwaka wanapokea wastani wa mashauri 800 .
Kwa upande wake Mtendaji Kata ya Igulwa eneo ambalo, Mahakama ya Wilaya ya Bukombe ilipo alisema anaishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma hiyo, ambayo ina nafasi kubwa , ikiwemo Mahakama ya Mwanzo ya Ushirombo, ambapo kwa sasa kila mtumishi ana chumba chake cha kufanyia kazi hali inayosababisha mashauri kumaliza saa 4.00 asubuhi na wananchi wanapata muda kuendelea na shughuli nyingine.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe lilizinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Desemba 19 mwaka jana.
Mahakama ya Tanzania kupitia Mapango Mkakati wake wa Miaka Mitano, ambao unasisitiza kwamba utoaji haki kwa wote na kwa wakati iliweka utaratibu wa muda wa kusikiliza shauri mahakamani katika Mahakama za Wilaya kuwa lisidi miezi 12 na Mahakama za Mwanzo lisikilizwe katika kipindi cha miezi sita.