Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Peter Msofe, amemuelekeza Mkurugenzi wa Masoko wa wizara hiyo kutuma wataalamu kwenda kujifunza mfumo wa Farmers Service Center (FSC), huku akiwataka wadau wa kilimo kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia programu ya Farm to Market Alliance (FtMA).
Akizungumza Novemba 26, 2026, jijini Dodoma wakati wa kufunga programu ya FtMA iliyoanzishwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Prof. Msofe amesema ni muhimu kuendeleza mifumo yenye mafanikio ili kuongeza tija, ubora na ushindani wa sekta ya kilimo nchini.
Amesema kilimo kinachoongozwa na mahitaji ya soko kinahitaji wakulima kupata taarifa sahihi za masoko ili waweze kuzalisha kulingana na mahitaji, kuongeza faida na kupata masoko ya uhakika. Aidha, amebainisha kuwa takribani asilimia 25 ya mazao hupotea kutokana na uharibifu, hivyo akasisitiza umuhimu wa uhifadhi na usindikaji.
Prof. Msofe ameeleza kuwa zaidi ya vituo 924 vya huduma kwa wakulima vimeanzishwa, ambapo vituo 108 vimefuzu na kutambuliwa, huku akiwataka wanufaika kusaidia vikundi vingine kuanzisha na kuimarisha vituo hivyo ili viweze kufikia viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, mfadhili wa programu hiyo, Phillip Hewitt kutoka New Zealand, amesema FtMA imekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha, wafanyabiashara na mashirika ya wakulima katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta ya kilimo
Amesema wakulima wanaendelea kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, misimu isiyotabirika ya mvua na kuyumba kwa bei za mazao, hivyo ni muhimu kuendeleza ushirikiano uliojengwa ili kuhakikisha mifumo ya chakula na fursa za kiuchumi zinakuwa endelevu.
Naye Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP nchini, Ronald Tran Ba Huy, amesema katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa FtMA mwaka 2016, programu hiyo imefanikiwa kuwaunganisha zaidi ya wakulima 250,000 na huduma za kilimo pamoja na fursa za kibiashara kupitia mtandao wa vituo vya huduma kwa wakulima.
Amesema programu hiyo imejenga ushirikiano na taasisi zaidi ya 250 za sekta ya umma na binafsi, huku vituo hivyo vikitoa huduma za pembejeo bora, mitambo ya kilimo, ushauri wa kitaalamu, huduma za kifedha na taarifa za masoko pamoja na kuwaunganisha wakulima na wanunuzi.
Aidha, amesema pamoja na programu ya FtMA kuhitimishwa, WFP itaendelea kuimarisha na kupanua mfumo wa vituo vya huduma kwa wakulima kupitia programu zake za ustahimilivu, maisha endelevu na mifumo ya masoko ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelea kudumu.
Programu ya FtMA ilianza kutekelezwa Tanzania mwaka 2016 na kufanyiwa maboresho mwaka 2021. Pia imetekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Rwanda, kwa kushirikiana na timu ya kimataifa ya FtMA.

