Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mbingu (Mlimba), yenye urefu wa kilometa 62.5, kuhakikisha anaanza kazi ya ujenzi ndani ya mwezi mmoja ili kuondoa kero ya usafiri na usafirishaji inayowakabili wananchi wa eneo hilo.
Agizo hilo amelitoa leo, Novemba 25, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mchombe, Mlimba, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, alipofika kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao na kuzitafutia ufumbuzi.
“Wananchi wanataka kuona kazi ikiendelea. Kwa sasa hakuna kisingizio, mkandarasi ameshalipwa fedha, nataka kuona anafanya kazi,” amesema Dkt. Mwigulu.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa atawasiliana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ifikapo Desemba 25, 2026, ili kupokea taarifa pamoja na picha zitakazoonesha mitambo ikiwa imeanza kufanya kazi katika eneo la mradi huo.
Ameeleza kuwa atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha barabara hiyo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na uzalishaji inakamilika kwa wakati, na kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema barabara ya Ifakara–Mlimba ni sehemu ya barabara ya Dumila–Kilosa–Mikumi–Ifakara–Mlimba hadi Njombe, ambayo Serikali imepanga kuijenga kwa awamu.
Amefafanua kuwa Awamu ya Kwanza ilihusisha ujenzi wa barabara ya Kidatu–Ifakara pamoja na daraja lake, ambayo tayari imekamilika.
Ameongeza kuwa Awamu ya Pili inahusisha ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5, ambapo mkandarasi ameshapatikana na mkataba wa ujenzi umesainiwa. Hata hivyo, kinachosubiriwa ni mkandarasi kuanza kazi katika eneo la mradi, huku tayari akiwa amelipwa takribani shilingi bilioni 9.5 kama malipo ya awali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.
Naye, Mbunge wa Mlimba, Dkt. Rose Rwakatare, amesema wananchi wa Mlimba wana kiu ya kuona ujenzi wa barabara hiyo ukianza na kukamilika kwa haraka ili kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji inayowakabili.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mlimba kwa kurahisisha shughuli za biashara na kilimo zinazofanyika katika jimbo hilo.

