NA DENIS MLOWE, IRINGA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeunga mkono wazo la barabara moja katika Manispaa ya Iringa kuitwa Edo Bashiri, kwa lengo la kumuenzi aliyekuwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, marehemu Edo Bashiri, kutokana na mchango wake katika siasa, uandishi wa habari na shughuli za kijamii.
Wazo hilo limetolewa na Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu, akieleza kuwa kutambua mchango wa watu waliolitumikia jamii ni sehemu muhimu ya kuendeleza kumbukumbu za kazi zao na kuwahamasisha wengine.
Ngajilo amesema marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa namna ya kumuenzi na kwa mkoa kutafuta barabara itakayobeba jina lake, ili kumbukumbu ya maisha na kazi zake iendelee kuwa sehemu ya historia ya mji wa Iringa.
Wazo hilo limeungwa mkono na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi aliyeagiza viongozi wa mkoa kuharakisha hilo na , alisema chama kimempoteza kiongozi mahiri, mwenye upendo na aliyekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za chama, hususan wakati wa kampeni za uchaguzi.
Kihongosi amesema anamkumbuka marehemu tangu miaka ya awali ya uandishi wa habari na shughuli za burudani, akieleza kuwa studio za AB Records zilizokuwa nyumbani kwao zilikuwa sehemu ya kukutana kwa vijana mbalimbali, wakiwemo DJ Nas, Temi Mahondo na Edo Bashiri, waliokuwa na ndoto za kukuza vipaji vyao.
Amesema chama kinatambua mchango wa marehemu katika kampeni na shughuli mbalimbali za kisiasa, huku akimshukuru Salim Abri Asas kwa namna alivyoshiriki katika kusaidia matibabu ya marehemu alipokuwa akiugua.
Aidha, Kihongosi ametangaza kuwa CCM kupitia Makao Makuu itatoa Sh milioni 10 kwa ajili ya watoto wa marehemu, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia katika kipindi hiki cha changamoto, huku chama na wadau wengine wakitakiwa kuendelea kuisimamia familia hiyo.
Kwa upande wake, Salim Abri Asas amesis8itiza umuhimu wa jamii kujenga utamaduni wa kusaidiana wakati watu wakiwa hai, badala ya kusubiri baada ya vifo vyao, akieleza kuwa marehemu Edo Bashiri alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakijitolea kusaidia wenye mahitaji, wagonjwa na watu waliokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Asas amewataka viongozi na wadau kuvunja utamaduni wa kusubiri mtu afariki ndipo aanze kuenziwa, akisisitiza kuwa msaada kwa watu wenye changamoto za kiafya na kijamii unapaswa kutolewa wakati wanauhitaji.
Pia amewataka viongozi wa CCM kuhakikisha familia ya marehemu inaendelea kupata msaada hata baada ya mazishi, akieleza kuwa mshikamano wa kweli haupaswi kuishia kwenye shughuli za msiba.
Maelfu ya wananchi wa mkoa wa Iringa walihudhuria kwa wingi katika mazishi ya Edo Bashiri aliyefariki Novemba 24 mwaka huu wakiongozwa Kenani Kihongosi sambamba na mcc Salim Asas.
