
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Mtambuka ya EALA, Dkt. Abdullah Makame akizungumza akifungua mafunzo hayo jijini Arusha
…………….
Na Happy Lazaro, Arusha
KAMISHENI ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) imeanza kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika matumizi ya lugha ya Kiswahili, hatua inayolenga kuimarisha mawasiliano kati ya wabunge hao na wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM).
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Novemba 23 hadi 25 mwaka huu katika Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, yanalenga kuongeza umahiri wa wabunge katika kuzungumza na kutumia Kiswahili wanapotekeleza majukumu yao ya kibunge.
Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Mtambuka ya EALA, Dkt. Abdullah Makame, amesema uelewa wa Kiswahili ni muhimu kwa wabunge kwa kuwa wanawakilisha wananchi kutoka mataifa mbalimbali ya Jumuiya hiyo na wanapaswa kuwa na uwezo wa kuwasiliana nao kwa urahisi.
Amesema umahiri wa lugha hiyo utawasaidia wabunge kutekeleza majukumu yao makuu ya kutunga sheria, kusimamia utekelezaji wa shughuli za Jumuiya na kuwawakilisha wananchi, huku ukiwawezesha kushiriki kikamilifu katika mijadala inayohusu maendeleo na mustakabali wa kikanda.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Bunge la Afrika Mashariki na KAKAMA unaolenga kuwajengea wabunge uwezo wa kutumia Kiswahili kupitia programu maalumu ya mafunzo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa KAKAMA, Dkt. Caroline Asiimwe, amesema Kiswahili kina nafasi kubwa katika kuimarisha ushirikiano na utangamano wa Afrika Mashariki, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa kikanda kukifahamu na kukitumia katika shughuli zao za kila siku.
Amesema mbali na kutumika katika mawasiliano mapana ndani ya Jumuiya hiyo, Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi za JAM na kinaendelea kupanua wigo wake wa matumizi kimataifa, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuongeza matumizi yake katika taasisi za kikanda.
Dkt. Asiimwe amesema wabunge wanapokifahamu na kukizungumza Kiswahili kwa kujiamini, wanapata fursa nzuri zaidi ya kuwasiliana na wananchi, kueleza vipaumbele vya kikanda na kuimarisha utambulisho wa pamoja wa Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa KAKAMA imeanza na Bunge la Afrika Mashariki katika kutekeleza programu ya kujenga uwezo wa taasisi za Jumuiya hiyo katika matumizi ya Kiswahili, huku mafunzo yakiendelea kwa njia ya mtandao baada ya kukamilika kwa vipindi vya ana kwa ana ili kuwawezesha washiriki kukamilisha mahitaji ya kuhitimu kozi hiyo.
Naye Katibu wa Bunge la Afrika Mashariki,Alex Lumumba Obatre amesema kujifunza Kiswahili kutawawezesha wabunge kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuwasiliana moja kwa moja na wananchi wa kawaida katika nchi wanachama.
Ameongeza kuwa , programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na MS TCDC iliyopo Arusha, ambayo inatoa mchango muhimu katika kujenga uwezo na kuwezesha mafunzo ya vitendo, huku wawezeshaji kutoka taasisi nyingine zinazoshirikiana na KAKAMA wakishiriki katika kufanikisha programu hiyo.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia kupunguza vikwazo vya lugha katika shughuli za Bunge la Afrika Mashariki, kuongeza ushirikishwaji wa wananchi na kuimarisha matumizi ya Kiswahili kama nyenzo muhimu ya mawasiliano na utangamano wa kikanda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Mtambuka ya EALA, Dkt. Abdullah Makame akizungumza akifungua mafunzo hayo jijini Arusha
