Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa msingi muhimu wa kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya Serikali mbili katika kutatua changamoto na kusukuma mbele masuala yenye maslahi kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 26 Novemba 2026, alipokutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, Ikulu Zanzibar, ambapo wamejadili masuala ya Muungano, mazingira na maeneo mengine ya ushirikiano.
Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mifumo ya mashauriano na uratibu ili kuimarisha utendaji wa Serikali na huduma kwa wananchi, huku akieleza manufaa ya ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano unaoendelea kuimarika katika kushughulikia masuala ya Muungano na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kitaifa.
Amesema mahusiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar yana mizizi ya kihistoria na kindugu inayodhihirishwa na mwingiliano wa wananchi katika biashara, shughuli za kiuchumi, familia na mahusiano ya kijamii.
Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa msingi huo ni nguvu muhimu katika kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa, hivyo Serikali zote mbili zina wajibu wa kuendelea kujenga mazingira yatakayowawezesha wananchi kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na Muungano.

