Jamii imetakiwa kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ili kuilinda jamii na kuwa na familia imara, jamii imara na taifa imara.Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Athuman Katimba, wakati akizindua Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga wa Kijinsia iliyofanyika tarehe 25 Novemba 2026 jijini Dodoma.
Naibu Waziri Katimba amesema Serikali katika kupambana na Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia imetekeleza programu na kampeni mbalimbali ikiwemo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legai Aid Campaign) na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (2024/25 – 2028/29).
Amesema Serikali pia imetekeleza afua mbalimbali za ulinzi wa Wanawake na Watoto dhidi ya Ukatili, ikiwemo Kampeni ya Kitaifa ya kulinda watoto dhidi ya matumizi ya mtandao, uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika Jeshi la Polisi, Vyuo Vikuu na vya Kati na Madawati katika sehemu za umma ili kutoa huduma kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Mipango, Programu na Kampeni hizi zinalenga kusaidia utekelezaji wa Dira 2050 ili kuhakikisha mtaji watu wa kuleta maendeleo unalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili” amesema Naibu Waziri Katimba.
Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakim Chacha Maswi amesema mapambano dhidi ya ukatili yanahusisha wadau mbalimbali ili kuongeza nguvu na kuondoa ukatili kwenye jamii, katika kuendana na utekelezaji wa Dira 2050 kupitia Jamii Ajenda 2050 ili kufikia Familia Imara, Jamii Imara na Taifa Imara.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Khatibu Kazungu amesema Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia inaunganisha wadau mbalimbali katika kupambana na suala hilo na kuwa suala hilo ni Ajenda ya mkoa kwa kushirikiana na wataalamu pamoja na Wadau mbalimbali, kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za Ukatili na kuhimiza uimarishaji mifumo ya ushirikiano wa Taasisi zinazohusika na kupambana na suala hilo.
Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi ya WILDAF Wakili Anna Kulaya amesema wadau mbalimbali wamejidhatiti katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinakomeshwa ndani ya jamii kupitia Kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na majukwaa mengine mbalimbali.
Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Kitaifa kwa mwaka 2026 yanafanyika kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba 2026 yakiongozwa na Kaulimbiu isemayo “Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa Imara Lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050”.

