Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhiwa tuzo ya shukrani kutoka kwa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026.(anayekabidhi ni Bw. Fadhil Hezekiah, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa na Viongozi mbalimbali akishiriki ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati akifungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026.

Washiriki mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhiwa zawadi maalum ya picha iliyochorwa na Mfamasia Deogratius Bukulu mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akiagana na washiriki wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), mara baada ya kufungua Mkutano huo, unaofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza, leo tarehe 25 Novemba 2026.

………….. 

MWANZA 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Afya kutathmini mahitaji ya wataalamu wa famasi ili kubaini maeneo yenye upungufu mkubwa na kupendekeza hatua za kuwaajiri kwa awamu kulingana na bajeti.  

Agizo hilo amelitoa leo, tarehe 25 Novemba 2026, alipofungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania katika ukumbi wa Kwatunza Beach, Jijini Mwanza. Amesema ujenzi wa vituo vya afya na ongezeko la vitanda vinapaswa kwenda sambamba na ongezeko la wataalamu wa kuhudumia wagonjwa. 

Aidha,  ameitaka Wizara ya Afya kushirikiana na Ofisi ya Rais – UTUMISHI kukamilisha maboresho ya ikama ili kutambua ubobezi katika kada za afya, ikiwemo famasi, na kuharakisha kazi ya kuanzisha Kurugenzi ya Dawa wizarani.  

Pia ameielekeza wizara hiyo kukipatia chama cha Wafamasia Tanzania  eneo mara moja kwa ajili ya kujenga kiwanda darasa cha dawa na kusimamia uunganishaji wa mifumo ya taarifa za afya, ili kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyokwisha kuyatoa kuhusu kuunganishwa kwa mifumo ya Serikali ambayo itaongeza ufanisi na kuleta tija katika utoaji Huduma hususani kwenye Sekta ya Afya 

Akizungumzia mwenendo wa Sekta ya Famasi nchini Makamu wa Rais amewataka wafamasia kuzingatia maadili ya taaluma, kushiriki katika tafiti za dawa asili na kushirikiana na Serikali kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya antibiotiki ili kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa.  

Amesema wastani wa upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma umefikia asilimia 89 kutoka asilimia 57 mwaka 2021, huku bajeti ya dawa ikiongezeka kutoka shilingi bilioni 200 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi shilingi bilioni 438 mwaka 2026/2027. 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali imetenga ekari 400 eneo la Mloganzila kwa ajili ya kongani ya viwanda vya dawa. Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa dawa nchini na kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje. Dkt. Samizi amesema viwanda sita vya dawa vinaendelea kujengwa na baadhi vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2027. 

Akiwasilisha risala ya Chama cha Wafamasia Tanzania, Rais wa chama hicho, Mfamasia Fadhil Hezekiah, amesema katika baadhi ya maeneo idadi ya wataalamu wa famasi hailingani na wingi wa wagonjwa wanaohitaji huduma. Ameomba mapitio ya ikama yazingatie majukumu ya sasa ya wafamasia, yakiwemo kutoa huduma katika kliniki za magonjwa sugu, kusimamia ugavi na kufuatilia usalama wa dawa. Pia amependekeza kuanzishwa kwa Kurugenzi ya Dawa katika Wizara ya Afya ili kuimarisha uratibu wa huduma za famasi. 

Hezekiah pia ameiomba Serikali kukipatia chama hicho  ardhi kwa ajili ya kujenga kiwanda darasa cha dawa kitakachotoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wataalamu wa famasi.  

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, awali akiwakaribisha washiriki katika mkoa huo, amesema hadi Septemba 2026 upatikanaji wa dawa mkoani Mwanza ulifikia takriban asilimia 93, huku utoshelevu wa dawa ukifikia asilimia 85.5.  

Amesema kati ya mwaka 2021 na 2025 Serikali ilitoa ajira kwa watumishi 1,718 wa kada mbalimbali za afya mkoani Mwanza. Kwa mujibu wa Hamduni, ajira hizo zimesaidia kupunguza upungufu wa watumishi wakati halmashauri zikiendelea kufungua vituo vipya vya afya. 

Kongamano hilo la siku tatu linafanyika kwa kaulimbiu “Mabadiliko ya Kizazi: Kujenga Uwezo wa Mfamasia Kuongoza Mageuzi katika Afya na Utengenezaji wa Dawa nchini Tanzania.” Likiwashirikisha Wafamasia, Wafamasia Wasaidizi, na Wadau wa Sekta ya Afya nchini.