Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Asha-Rose Migiro, kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wawili wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ndogo ya makao makuu CCM, Lumumba, jijini Dar es salaam.

Mabalozi hao ni Mheshimiwa Yordenis Despaigne Vera, Balozi wa Jamhuri ya Cuba na Mheshimiwa Vu Thanh Huyen, Balozi wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam, wote wenye makaazi yao nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya CCM na vyama rafiki vya CPC–Cuba na CPV–Viet Nam, hususan katika maeneo ya uongozi, mshikamano wa vyama vya siasa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Migiro, alifanya mazungumzo na Mheshimiwa Susan Ngongi Namondo, Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, ambapo walijadiliana vipaumbele vya maendeleo ya jamii katika utekelezaji wa baadhi ya maeneo yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 ambayo yanawiana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na Malengo ya Maendeleo ya Kimataifa (SDGs).