*Kumuwakilisha Rais Dkt. Samia mkutano wa ushirikiano wa Afrika na Ufaransa
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Mei 10, 2026 amewasili Nairobi, Kenya ambako anatarajia kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Ushirikiano wa Afrika na Ufaransa (Africa Forward: Africa–France Partnership for Innovation and Growth Summit) utakaofanyika Mei 11–12, 2026.
Lengo la mkutano huo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, teknolojia, nishati, afya, Akili Unde (AI), kilimo, uchumi wa buluu pamoja na viwanda.
Aidha, mkutano huo unalenga kukuza uwekezaji mpya kati ya Afrika na kampuni za Ufaransa, kujenga ushirikiano unaotajwa kuwa wa usawa, pamoja na kujadili mageuzi ya mfumo wa fedha na maendeleo endelevu ya Afrika.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali unawakutanisha wadau wa maendeleo, wawekezaji pamoja na sekta binafsi, na umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa William Samoei Ruto, na Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Mheshimiwa Emmanuel Macron.

