***********************
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi amewataka wamiliki na wafanyabiashara wa Hoteli Jijini Dar es salaam kutumia fursa ya kibiashara itakayotokana na ujio wa wageni takribani 1000 watakaoshiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia mwezi August 2019.
Waziri Prof Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli na kuongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itafanya kazi kwa ukaribu na wadau hao wa Hoteli na kuwataka kutoa huduma bora,bidi,weledi na kwa uzalendo usiotiliwa mashaka ili waweze kunufaika na uwepo wa ugeni huo mkubwa wa SADC.
“Ninyi ni watu muhimu sana katika ugeni huu wa SADC,tushirikiane kuufanya mkutano huu kuwa wa mafanikio makubwa kwa ukarimu na uzalendo wetu na hivyo kutufanya pia kuingiza kipato katika biashara zetu kwa kuwa tukifanya vizuri kila watakapokuwa wanakuja Tanzania kwa mikutano mingine ya mawaziri watafikia katika hoteli zetu kutokana na ukweli kuwa tutakuwa na mfululizo wa mikutano ya SADC kuanzia August 2019 hadi August 2020 Tanzania itakapokoma kuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo”
Ameongeza kuwa ataendelea kukutana na wadau mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wa Sekta binafsi ili kuhakikisha fursa ya kufanyika kwa mkutano wa SADC hapa nchini inawanufaisha pia wadau mbalimbali wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara.
Katika Mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi ameongozana pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo kwa upande wake amesema kutokana na Mkutano huo wa SADC serikali inatarajia kuingiza zaidi ya shilingi bilioni kumi pamoja na kutengeneza ajira zaidi ya elfu tano na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo.
Pia amewataka wamiliki na wafanyabiashara hao wa hoteli kuzingatia muongozo wa serikali uliotolewa na Gavana wa benki kuu ya Tanzania kuhusiana na suala la ubadilishaji wa fedha za kigeni kwa kuwataka kuwaelekeza wageni kubadilishia fedha zao benki na pia katika hoteli ambazo zimeidhinishwa kubadilisha fedha za kigeni.