Dkt. Analice Kamala akifafanua mada kwa wanahabari katika mafunzo ya usalama wa chakula ulioandaliwa na mamlaka ya chakula na dawa nchini tfda
*************************
Na Grace Semfuko,MAELEZO
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA imesema inayo maabara ya
kisasa ya upimaji wa usalama wa mazao ya Chakula ili kuondokana madhara
yatokanayo na ulaji wa vyakula vizivyopimwa yakiwepo magonjwa
yanayotokana na ulaji wa vyakula vyenye Sumu kuvu.
Aidha Mamlaka hiyo imejipanga kupambana na magonjwa yanayosababishwa
na ulaji wa vyakula hivyo ambayo yana athari kubwa kwa afya za binaadamu
ikiwepo udumavu na vifo.
Hayo yalibainishwa na Mkaguzi wa chakula Mwandamizi wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa Tanzania TFDA Dkt Analice Kamala wakati akiwasilisha
mada juu ya uchafuzi wa Sumukuvu madhara yake kwa afya na jinsi ya
kudhibiti katika Semina ya kuwajengea uwezo Waandishi na Wahariri wa
Habari katika kuelimisha jamii kuhusu usalama wa chakula iliyofanyika
Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.
Dkt Kamala alisema alisema maabara za kisasa za upimaji wa vyakula
zilizopo kwenye Mamlaka hiyo zina uwezo wa kisasa wa kubaini magonjwa
au vimelea vya fangas ambavyo huathiri vyakula hususa vilivyohifadhiwa
kwenye maeneo yasiyo salama ikiwepo sehemu ya unyevu unyevu,joto na
wadudu wa nafaka.
“ Niwahakikishie tu watanzania wenzangu kuwa vyakula vinavyopimwa
kwenye maabara hii ni salama, hakuna kinachopita hapa kikiwa na madhara,
kitatupwa tu, tuzingatie usalama wa vyakula na tutumie vyakula
vilivyopimwa alisema Dkt Kamala.
Aidha katika hatua nyingine Dkt Kamala aliwataka Wanawake
wanaonyoshesha nchini kuwa waangalifu katika uandaaji na matumizi ya
vyakula wanavyotumia ili kuepukana na madhara ya Sumukuvu iliyopo
kwenye baadhi ya vyakula vya nafaka ambayo inadaiwa kuwa na madhara
kwa binaadamu na wakati mwingine husababisha vifo.
Dkt Kamala alisema iwapo Mama anayenyonyesha atatumia vyakula vyenye
sumukuvu anasababisha madhara makubwa kwa Mtoto ikiwepo Udumavu,
Vifo na Magonjwa ambayo yanaathiri ukuaji wa mtoto.
“Wanawake wanaonyonyesha ni muhimu kuzingatia uandaaji wa vyakula
kwani watoto hula vyakula hivyo kupitia kwenye Maziwa ya Mama na hivyo
kuathiri mfumo mzima wa ukuajiälisema Dkt Kamala.
Aidha pia Dkt Kamala alisema ulaji wa mazao ya mifugo iliyotumia vyakula
vilivyoathiriwa na sumu kuvu pia inaweza kuathiri afya za binaadamu.
Alisema Sumu kuvu inaathiri ini na Figo na kusababisha ugonjwa wa manjano
na wakati mwingine kuvuja damu kwenye maeneo ya wazi,kuharisha na
kuhisi kichefuchefu na dalili zake huanza kuonekana baada ya wiki mbili.
Ugonjwa huo kwa Nchini Tanzania ulilipotiwa na Wizara ya Afya Juni 13
mwaka 2016 Mkoani Dodoma ambapo ilibainika kuwepo kwa watu 68 kwenye
familia 42 kuugua magonjwa yatokanayo na ulaji wa vyakula vyenye sumu
kuvu na kati yao watu 20 sawa na asilimia 30 walipoteza maisha.