WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. George Simbachawene,akizungumza na watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria mara baada ya kutembelea banda hilo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendeleza juhudi za kutatua migogoro katika jamii kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Simbachawene ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea  banda la Wizara hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

“Ukitaka kuhakikisha kuwa maendeleo yapo ni lazima tuhakikishe hakuna migogoro. Kama ni kesi tayari zilishakuwepo mahakamani, lakini jitihada kubwa mmezifanya na sasa mmechochea amani na upendo katika jamii,” amesema Simbachawene.

Aidha, amesema juhudi hizo zimechangia kupunguza malalamiko na migogoro katika jamii, hali iliyosaidia kuimarisha utulivu na kurahisisha maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mbaraka Stambuli, amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imelenga kuwasaidia wananchi wasioweza kumudu gharama za mawakili au kuandaa nyaraka za kisheria.

“Kampeni hii inahakikisha kila mwananchi anapata haki yake. Mpaka sasa tumeweza kuwafikia wananchi milioni tatu Tanzania Bara na Visiwani, na tunatarajia kuja na awamu ya pili ya kampeni hii,” amesema Mbaraka.