Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia ,William Ole Nasha akizungumza katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Ufundi Arusha ambapo jumla ya wahitimu 436 wametunukiwa Astashahada ,Stashahada,Shahada ya juu na shahada
Wahitimu wa ngazi mbalimbali chuo Cha ufundi Arusha wakiwa katika mahafali yao yaliyofanyika hiii Leo chuoni hapo.
Baadhi ya wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali Mara baada ya kutunukiwa vyeti vya Leo chuoni hapo
(Happy Lazaro)
………………….
Happy Lazaro,Arusha
Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia ,William Ole Nasha amewataka vijana wanaohitimu vyuo vya ufundi kujikita katika kuanzisha ajira mpya kwa kujiajiri badala ya kusubiria nafasi chache za ajira zilizopo na hivyo watumie ujuzi wao na taaluma kuisadia jamii.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Ufundi Arusha ambapo jumla ya wahitimu 436 wametunukiwa Astashahada ,Stashahada,Shahada ya juu na shahada.
Ole Nasha amewataka wahitimu hao kuwa na udhubutu wa kuanzisha ajira zao wenyewe hata katika kiwango cha chini kwani zitaweza kukua na kuwafanikisha malengo yao.Nasha amewataka wahitimu hao wasikae majumbani wakisubiri ajira bali waanzishe miradi midogo midogo itayowasaidia na kusaidia jamii zao ,hivyo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.“mafanikio katika maisha yenu hayatategemea tu elimu ya ufundi bali yatatokana na nidhamu na uthubutu .Ninafahamu zipo changamoto katika kujiajiri lakini muhimu kuliko yote ni kuwa na nia na uthubutu .Eneo la ufundi lina fursa nyingi sana”alisema Naibu Waziri wa Elimu.
Balozi wa Norway nchini Tanzania ,Elisabeth Jacobsen amesema kuwa, Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha elimu ya Ufundi ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda kama iliyo adhma ya serikali.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ,Dr.Masudi Senzia amesema kuwa ,chuo hicho kimeongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika masomo ya kike kutokana na idadi ndogo ya vijana wa kike wanaojiunga na elimu ya Ufundi .
Masudi ameiomba serikali iwapatie fedha za kujenga shule za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike ambao asilimia kubwa wanaishi nje ya chuo.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC),Chacha Makamba Wambura amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha elimu ya ufundi na kujenga miundombinu rafiki na vifaa vya kisasa vya kujifunzia suala linalopelekea kupata wahitimu waliobobea katika fani zao.