Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumu na Uwekezaji Khamis Suleiman Mwalim (Shibu) wakati alipokuwa akifunguwa Mafunzo ya Waandishi wa Habari kuhusu Kamisheni ya Kazi huko katika Ukumbi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mayugwani Zanzibar.
By: Takdir Ali.
MAELEZO YA PICHA.
Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumu na Uwekezaji Khamis Suleiman Mwalim (Shibu) amewataka Waajiri nchini kuwapa Mikataba Wafanyakazi wao ili kutii matakwa ya Kisheria.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunguwa Mafunzo ya Waandishi wa Habari kuhusu Kamisheni ya Kazi huko katika Ukumbi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mayugwani Zanzibar.
Amesema suala la Mikaba ni suala la Sheria hivyo Waajiri kuwafanyisha kazi Wafanyakazi wao bila Mikataba ni kosa kwa mujibu wa Sheria.
Amesema kuna baadhi ya Wafanyakazi hasa wa sekta binafsi wanapata matatizo mengi ikiwemo ya kufanya kazi bila Mikataba hivyo amewataka Waandishi wa Habari kushirikiana na Kamisheni ya Kazi kutoa elimu ya Sheria za Kazi kwa Wafanyakazi na jamii.
Kwa upande wake Kamishna wa Kazi kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Rashid Khamis Othaman amesema Kamisheni ya Kazi imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupanda Mishahara, kutoa Mikataba ya Ajira 37,455 kwa Unguja na Pemba.
Aidha amesema mafanikio mengine yalipatikana ni pamoja na kusuluhisha na kutatua Migogoro ya Kazi 636 kati ya 743 ilipokelewa.
Nao Waandishi wa Habari walioshiriki katika Mafunzo hayo wamesema wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo kukosa Mikataba na kulipwa Mishahara kinyume na maelekezo yaliotolewa na Serikali.
Hivyo wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kuandaa utaratibu wa kukutana na Waajiri wa vyombo vya habari ili kuweza kuondosha Changamoto zilizopo.