Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa afisa wa TBA Haruna Kalunga (kulia) wakati alipotembelea ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya kalambo.
***********************************************
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura amemkaribisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo katika ofisi yake mpya anayotarajia kuhamia mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka 2019 huku ikiwa zimebaki asilimia 10 kumalizika kwa jengo hilo tofauti na ofisi ya mpya ya Mkurugenzi ambayo bado ipo katika hatua za awali za ujenzi.
Mh. Binyura aliwashukuru wakandarasi Suma JKT pamoja na mshauri wake wakala wa majengo Nchini (TBA) kwa kuweza kuifikisha ofisi hiyo katika hatua za mwisho kuongeza kuwa pamoja na yeye kuhamia pia anaweza kushirikiana na mkurugenzi kukaa pamoja ikiwemo kumuazima mabanda yanayozunguka ofisi hiyo ili aweze kuyatumia wakati wakisubiri kukamilisha ofisi yao.
“Ni kweli jengo hili ni kubwa sana na ofisi hii itatosha kwa ofisi yangu pia na Mkurugenzi ataingia na pia kuna mabanda mengi tu yapo hatutayabomoa mapema ili waweze kuingia lakini vile vifaa ambavyo ni vya kutumia mifumo wataingia kwenye jengo langu, kwahiyo nawakaribisha sana na wajenzi wajitahidi ili tarehe 30 niweze kuingia kwenye jengo hili,” alisema.
Kauli hiyo imekuja baada ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kumtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhama katika madarasa ya shule ya Sekondari ya wasichana Matai ambayo wanayatumia kama ofisi zao.
Mh. Wangabo alisema,” Mh. DC nimesema hawa halmashauri ofisi zao zitahamia kwako kwa muda utakapokuwa umehamia pale na pale uwape muda wa kukaa ili uwasukume watoke pale, kama hawatasimamia huu ujenzi hapa wake kule kwenye vibanda vya kuku kule,wakae kweny vibanda vya mabati ili waone uchungu wa kusimamia hapa mahali.
Mh. Wangabo aliyasema hayo alipotembelea ujenzi wa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Ofiri ya Mkurungenzi wa halmashauri pamoja na ujenzi wa bwalo na mabweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Matai.
Katika hatua nyingine Mh. Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Kalambo kuhakikisha hadi kufikia mwezi Julai mwaka 2019 shule hiyo iwe imesajiliwa na kuanza kupokea wanafunzi kutoka katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo mwaka 2012 Mkurugenzi amekuwa akitumia madarasa ya shule ya sekondari ya wasichana ya Matai kama ofisi za halmashauri.