Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza na Mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo. Mazungumzo yao yamefanyika tarehe 04 Oktoba 2024 jijini Maputo. Uchaguzi wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji utafanyika tarehe 09 Oktoba 2024.
…..
Rais Mstaafu wa Zanzibar na
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume ameendelea
kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji ambapo tarehe 04
Oktoba, 2024 jijini Maputo amekutana na kufanya mazungumzo na Mgombea urais wa
Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.
Katika mazungumzo yao,
Mhe. Chapo alimweleza Mhe. Dkt. Karume masuala mbalimbali kuhusu maandalizi ya
chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika
nchini humo tarehe 09 Oktoba 2024.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Karume alimshukuru Mhe. Chapo kwa taarifa yake na kumweleza lengo la Misheni anayoiongoza kuwa ni kuangalia uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021 na kuridhiwa na nchi wanachama. Pia alitumia nafasi hiyo kuwatakia wananchi wa Msumbiji uchaguzi mwema wa amani na utulivu.
Wakati wa Mkutano huo,
Mhe. Dkt. Karume aliambatana na Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania, Zambia na
Malawi, Sekretarieti ya SADC akiwemo Mwenyekiti wa Troika, Prof. Kula Ishmael Theletsane
na
Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala
ya Uchaguzi la SADC (SEAC). Wajumbe wa
Troika kutoka Tanzania walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na
Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema.
Mhe. Dkt. Karume kwa
nafasi yake ya Mkuu wa Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC ameendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambapo
hadi sasa amekutana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Mabalozi
wa Nchi za SADC waliopo Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji na
Kamishna Msidizi wa Jeshi la Polisi la Msumbiji.
Mazungumzo yakiendelea ambapo Mhe. Chapo amemweleza Mhe. Dkt. Karume kuhusu maandalizi ya uchaguzi ya Chama chake kuelekea uchaguzi tarehe 09 Oktoba 2024 |
Mhe. Chapo akizungumza |
Wajumbe wakishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani). |
Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume akiagana na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo baada ya kumaliza mazungumzo yao |
Picha ya pamoja |