Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto,
Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma wa kwanza
kushoto, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mkoa wa Lindi Peter
Ludovick mwenye suit ya Blue na Mhandisi kutoka tume ya Madini
Fadhili Kitivai wakitoka kwenye machimbo ya madini ya Gypsum ya
kampuni ya KNAUF Tanzania Ltd mkoani Lindi.
Faridu Sheweji mchimbaji mdogo wa madini ya Gypsum wilaya ya
Kilwa akitoa maelezo kwa mwenyekiti na Kamishna wa Tume ya
Madini Prof. Kikula Katikati na Prof. Mruma wa kwanza kulia kuhusu
shuguli zake alipotembelewa kwenye eneo lake la machimbo.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya KNAUF Tanzania Ltd Georgios
Zachopoulos wa tatu kushoto akitoa maelezo kwa Mwenyekiti na
Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto na Prof. Abdulkarim Mruma wa kwanza kushoto wakiwa kwenye eneo la
machimbo. Wa tatu kulia ni Afisa Madini Mkazi mkoa wa Lindi
Mhandisi Jeremiah Hango.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Kikula kushoto akikagua baadhi
ya kifaa kinachotumika kufanyia tathmini ya thamani ya madini wakati
wa mauzo ya madini kwenye soko la madini mkoa wa Mtwara lililopo
kwenye jengo la Afisa Madini Mkazi Mtwara. Kushoto ni Kamishna
wa tume hiyo Prof. Abdulkarim Mruma.
*****************************
Na Issa Mtuwa (Wizara ya Madini) Lindi na Mtwara
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amekutana na kilio cha
wachimbaji wa madini mkoani Lindi kuhusu ongezeko la tozo zilizo
kinyume cha sheria ya madini. Wakiongea kwa nyakati tofauti wachimbaji
hao wamesema halmashauri za wilaya na vijiji zimekuwa zinawatoza tozo
zaidi na ile iliyowekwa na sheria mama ambayo ni 0.03 badala yake
wamekuwa wakitumia sheria ndogo (by law) zilizopitishwa na baraza la
madiwani kuwatozo tozo zadi kinyume na sheria mama.
Wameongeza kuwa halmashauri zinatoza tozo zao, na halmashauri za vijiji
nazo zinajipangia ushuru wao kitu ambacho kina kuwa kero na
kusababisha usumbufu kilio ambacho walikiwasilisha wakati wa mkutano
mkuu wa sekta ya madini uliofanyika tarehe 22/01/2019 chini ya uenyekiti
wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Prof. Kikula amekutana na kilio hicho akiwa ziara mkoani humo kutembelea
na kukagua shuguli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wadau wa
madini. Kufuatia kilio hicho, Prof. Kikula ametoa wito kwa wachimbaji wa
madini ya Gypsum, Kokoto, Chumvi na mchanga nchini kote kuwa na
subira wakati Tume ya Madini ikihangaikia utatuzi wa changamoto hiyo ya
utozwaji wa tozo zinazo tozwa na baadhi ya halmashauri za wilaya na vijiji
kinyume na taratibu za sheria ya madini.
Prof. Kikula ameyasema hayo leo mara baada ya kutembelea machimbo
mbalimbali ya madini ya Gypsum ikiwemo ya kampuni ya KNAUF Gypsum
Tanzania Ltd, machimbo ya Mavuji yanayomilikiwa na mchimbaji mdogo
Faridu Sheweji na mchimbo ya chumvi yanayomilikiwa na Magereza Lindi
eneo la Machole.
Akijibu hoja ya kero hiyo, mwenyekiti wa tume amekiri uwepo wa
malalamiko ya namna hiyo kutoka kwa wachimbaji wa mikoa mbalimbali
nchini na siyo kwa Lindi peke yake. Anashangazwa na hali hiyo kwa kuwa
sheria ya madini na miongozo mbalimbali iko wazi na inaelekeza vizuri
kuhusu tozo zinazotakiwa kutozwa. Amesema wao kama tume wanafanya
jitihada kutatua kero hiyo, hivyo watawasilisha malalamiko yao kwa
mamlaka ya juu ambayo ni Waziri mwenye dhamana ya madini Doto Biteko
ili aweze kuzungumza na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mita
(TAMISEMI) Suleiman Jafo ili kuondoa kero hiyo.
“Nalitambua hili tatizo, kila tunapofanya ziara mikoa mbalimbali hii
changamoto inajitokeza, sijui ni kwa nini inakuwa hivyo kwa sababu sheria
iko wazi namna tozo zinavyotakiwa kutozwa. Naomba niwaahidi
tutalishugulikia hili haraka sana, na mara baada ya ziara hii tutaandaa ripoti
na kuiwasilisha kwa Waziri Biteko, pamoja na ripoti lakini pia nitamwambia
kwa mdodomo ili kusisitiza juu ya kero hii” amesema Prof. Kikula.
Prof. Kikula ameziomba halmashauri na kila mdau wa madini kote nchini
wazisome na kuzipitia vizuri sheria ya madini hususani inayohusu tozo
mbalimbali za madini kabla ya kuanza kuwatoza wachimbaji. Mwenyekiti
ameambatana na Kamishna wa Madini Prof. Abdulkarim Mruma walio anza
ziara ya kikazi katika mikoa minne ya Lindi, Ruvuma, Njombe na Iringa
katika kukagua shuguli za madini na kusikiliza na kutatua kero.
Wakati huo huo mwenyekiti wa Tume ya Madini amefanya mazungumzo
na wafanyakazi wa Tume hiyo wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye ofisi
za Afisa Madini Mkazi mkoa wa Mtwara. Amesikiliza kero za wafanyakazi
hao hususani ukosefu wa watumishi na vitendea kazi. Kuhuusu magari
amesema katika mwaka wa fedha ujao kila mkoa utapata gari jipya
kuongezea yaliyopo na kuhusu watumishi suala hilo linafanyiwa kazi.
Amewakumbusha kuhusu uadilifu katika kazi zao.