Mwenyekiti wa TCCIA Gabriel Kenene akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maonesho ya 19 ya wafanyabiashara ya Afrika Mashariki yatakayoanza Septemba 6 hadi 15 mwaka huu
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza Gabriel Kenene (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maonesho ya biashara ya Afrika Masharikiakiwa kulia ni Katibu mtendaji Hassan Kalambi.
……………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yamepangwa kuanza Septemba 6 hadi 15, 2024 katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 4, 2024 na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene wakati akitoa taarifa ya kuanza kwa maonesho hayo kwa waandishi wa habari.
Amesema idadi ya makampuni yanayotarajiwa kushiriki katika maonesho hayo ni 235 ambapo 200 ni kutoka ndani ya nchi na 35 ni ya nje ya nchi.
“Makampuni mbalimbali ya binafsi na umma,idara za Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii ni miongoni mwa makampuni yanayotegemewa kushiriki katika maonesho hayo,mwaka uliopita maonesho yalitembelewa na watu wapatao 250,000 kutoka Mkoa wa Mwanza na miji inayozunguka Jiji la Mwanza tunategemea idadi hiyo kuongezeka mwaka huu kufikia watu 300,000”, amesema Kenene
Akizungumzia malengo ya maonesho hayo Kenene amesema ni kutoa fursa kwa makampuni ya Tanzania na Afrika Mashariki katika kujitangaza,kutoa fursa kwa jumuiya ya wafanyabiashara kuimarisha mtandao wa masoko na usambazaji wa bidhaa zao pamoja na kutoa fursa kwa makampuni ya Tanzania kujifunza na kupanua wigo wa biashara za nje kwakutumia fursa zilizopo za makubaliano ya kibiashara kati ya Tanzania na nchi zingine kama EAC,SADC,AGOA,na EBA.