JOHN BUKUKU, DODOMA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imejipanga kuwasaidia Wajasiriamali nchini kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS) pamoja Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS) ikiwa na lengo la kuwezesha sekta binafsi wenye miradi mizuri kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha zilizosajiliwa chini na Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha2006, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana.
Akizungumza leo Agusti 5, 2024 katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika Nzuguni jijini Dodoma, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Gloria Samwel Chellunga, amesema kuwa BoT wanasimamia mfuko wa udhamini wa mkopo kwa niaba ya serikali ili kuwasaidia watanzania kupata mitaji kuongeza uzalishaji, ajira, fedha za kigeni na pato la Taifa kwa ujumla.
Chellunga amesema kuwa mfuko wa udhamini wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati una lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati wenye miradi mizuri lakini wana upungufu wa dhamana, kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu.
Amesema kuwa mfuko huu unatoa udhamini usiozidi asilimia 50 kwa mikopo kati ya shilingi milioni 50 hadi shilingi bilioni moja itakayotolewa kwa kipindi kati ya mwaka 1 hadi 5.
Amesema kuwa Mfuko wa Udhamini wa mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi umelenga kuwezesha wakopaji wenye miradi mizuri kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa na mauzo nje ya nchi, kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana.
Ameeleza kuwa udhamini wa mikopo katika mfuko huu hauzidi asilimia 75 kwa mkopo unaolipika ndani ya mwaka mmoja; na asimilia 50 ya mkopo kwa mkopo unaolipika zaidi ya mwaka mmoja.
“Kwa mkopo wa mazao ambayo mzunguko wa uzalishaji na uuzaji wake unazidi miezi kumi na mbili (12) lakini si zaidi ya miezi kumi na tano (15), udhamini wa mkopo hautazidi asilimia 75” amesema .
Amesema kuwa lengo ni kusaidia sekta binafsi pamoja na wajasiriamali wadogo na wa kati wenye miradi mzuri ila wana upingufu wa dhamani kupata mikopo kutoka benki au taasisi za fedha zinazosimamiwa na benki kuu.
Amesema kuwa ili uweze kupata dhamana katika mifuko huo, mwombaji ambaye ni mjasiliamali akiwemo mvuvi au mkulima anatakiwa kutuma maombi katika benki yake akiwa na andiko linaloelezea mradi wake.
Amefafanua kuwa benki au taasisi ya fedha itafanya tathmini ya mkopo huo kwa kuzingatia sera yao ya mikopo. Benki husika ikiridhia kumkopesha ila ikathibitika kuwa hana dhamana toshelevu, benki hiyo itatuma maombi BoT kwa ajili ya kupata dhamana kwa ajili ya kumkopesha mteja wake.