Na John Bukuku, Ikulu Dar es Salaam
……………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezipongeza taasisi ambazo zimefanikiwa kutoa gawio na kwamba zimethibitisha kuwa sera, miongozo na mazingira yaliyowekwa na serikali yamewawezesha kufanya kazi na kuzitaka taasisi zingine kufuata njia hiyo.
Amesema amepokea magaiwo makubwa kutoka taasisi ambazo serikali ina hisa chache, hivyo ni ujumbe kwa taasisi za serikali kuongeza kasi ili kufikia mafanikio.
Rais Samia amesema hayo leo Ikulu Dar es Salaam wakati akipokea gawio la Shilingi bilioni 637 kutoka kwenye mashirika na taasisi 145 kati ya 304 zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi na zile ambazo serikali ina hisa na kusimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Tumeona Benki ya NMB, Kampuni ya Twiga Mineral Corporation, Airtel Tanzania, Puma Energy na TPC Moshi wametoa gawio kubwa na sisi tuna hisa chache nadhani kila shirika lifanye kazi kwa juhudi ili kufikia kampuni hizi,” alisema. Mh. Rais Samia
Aidha, Rais Samia amesema kilichofanywa na Mashirika ya Umma kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Wakala wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC) na BRELLA ni ushahidi tosha wa kuweka mifumo mizuri na kushirikisha wawekezaji.
“Wapo ambao walipiga kelele kwamba Ooh.. mama anauza bandari, lakini gawio la Shilingi bilioni 153.9 ya TPA ni matokeo ya wawekezaji ambao wapo pale imani yangu ni mwakani wataongeza,” amesema.
Kuhusu mifumo kusomana Rais Samia ameagiza mamlaka husika kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu mifumo iweze kusomana na kwamba suala hilo limechukua muda mrefu. ambapo ameongeza kuwa hataki kusikia shirika ambalo mifumo yake haisomani na mingine.
Kiongozi huyo amesema alipoingia madarakani aliagiza mashirika ya umma na taasisi ambazo serikali ina hisa zibadilike na kuchangia katika pato la taifa, jambo ambalo limeanza kutekelezwa.
Awali akitoa taarifa yake mbele ya Rais Samia, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema ofisi yake inaendelea kusimamia mageuzi ya mashirika na tija imeanza kuonekana.
Mchechu amesema sheria inayosimamia ofisi ya Msajili wa Hazina inaelekeza mashirika kutumia si zaidi ya silimia 60 ya mapato yake iliyoyakusanya na kutoa gawio kwa serikali ambapo hadi sasa zaidi ya taasisi 145 zimetoa huku 159 zikitarajiwa kutoa kati ya 304.
Aidha, ameongeza kuwa taasisi zote zimeingia mkataba wa utendaji kazi kati ya bodi zao na ofisi ya Msajili wa Hazina na kwamba wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kuripoti taarifa za utendaji wa watendaji wa wakuu wa taasisi.
Msajili huyo amesema hadi kufikia Mei 2024 ofisi yake ilikuwa imepokea gaewio la Shilingi bilioni 637 ambapo Shilingi bilioni 279 kutoka ya mashirika ya biashara na Sh bilioni 358 ni taasisi za umma.
“Lengo letu ni kupokea gawio Shilingi bilioni 850, ila kwa sasa tumepokea Shilingi bilioni 637 kutoka taasisi 149 kati 159 imani yetu hadi mwisho wote watatoa,” amesema Mchachuko.