Afisa Madini Mkazi wa Chunya, Godson Kamihanda akizungumza kupitia mahojiano maalum kwenye maandalizi ya kipindi maalum chenye kuelezea mafaniko ya Sekta ya Madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa kinachoandaliwa na Wizara ya Madini, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO tarehe 02 Desemba, 2019 Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
Mthaminishaji wa Madini wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Chunya, Dickson Makwesa akipima madini ya dhahabu kwenye Soko la Madini Chunya mkoani Mbeya tarehe 02 Desemba, 2019
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli akielezea mchango wa Soko la Madini Chunya kwenye halmashauri yake.
………………………
Lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka 2019-2020 Chunya lafikia asilimia 91
Wanyabiashara wa Madini waipongeza Wizara ya Madini, Tume ya Madini
Greyson Mwase na Nuru Mwasampeta
Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya lililopo mkoani Mbeya mapema Mei 02, 2019 kumepelekea mabadiliko makubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Chunya ambapo kwa sasa wanakusanya wastani wa shilingi bilioni 1.09 kwenye biashara ya dhahabu tofauti na awali ambapo walikuwa wanakusanya kiasi cha shilingi milioni 114.9 kenye biashara ya dhahabu.
Hayo yalielezwa leo tarehe 02 Desemba, 2019 na Afisa Madini Mkazi wa Chunya, Godson Kamihanda kupitia mahojiano maalum kwenye maandalizi ya kipindi maalum chenye kuelezea mafaniko ya Sekta ya Madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa kinachoandaliwa na Wizara ya Madini, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO.
Kamihanda alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya kulikuwepo na utoroshwaji mkubwa wa madini kutokana na wafanyabiashara wa madini hayo kuuza kwa kificho na kukwepa kulipa kodi mbalimbali serikalini.
Alisema kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa soko husika na kufanya uhamasishaji wa matumizi ya soko, wafanyabiashara wengi wa madini walianza kuomba leseni za biashara ya madini na kuanza kufanya biashara mara moja.
Alifafanua kuwa, uwepo wa soko la madini umesaidia kwa kiwango kikubwa kwa ofisi yake kufikia kwa asilimia 91.2 ya lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambapo mpaka sasa wameshakusanya shilingi bilioni 17.33 kati ya lengo lililowekwa la shilingi bilioni 18.86.
Aliongeza kuwa, ili kuimarisha uendeshaji wa Soko la Madini Chunya, kumefunguliwa vituo vitano vya ununuzi wa madini ambapo wafanyabiashara wadogo wa madini hununua na baadaye huyauza kwenye Soko kubwa la Madini
“Hii tulifanya kama njia mojawapo ya kusogeza huduma kwa wafanyabiashara wadogo wa madini na kuongeza ukusanyaji maduhuli huku Serikali ikidhibiti utoroshwaji wa madini,” alisema Kamihanda.
Akielezea mikakati ya uboreshaji zaidi wa ukusanyaji wa maduhuli unaofanywa na ofisi yake, Kamihanda alisema kuwa ni pamoja na kufungua vituo zaidi vya ununuzi wa madini ya dhahabu pamoja na usajili wa mialo ya kuzalisha dhahabu kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji.
Aliongeza kuwa mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini na kuwataka wafanyabiashara wa madini kutumia Soko la Madini Chunya pamoja na vituo vilivyoanzishwa ili kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi na kupata faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli akielezea mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Soko la Madini Chunya, mbali na kumpongeza Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini alieleza kuwa uwepo wa soko hilo umeleta mabadiliko makubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwenye halmashauri husika.
Alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, halmashauri yake ilikuwa ikipanga kukusanya kiasi cha shilingi milioni 22 kwa mwaka na kufanikiwa kukusanya wastani wa shilingi milioni 19 tu.
Alisisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya hadi kufikia tarehe 21 Novemba, 2019 halmashauri ilikusanya kiasi cha shilingi milioni 278 ambazo zitatumika kuboresha huduma za jamii kama vile barabara, shule, maji, n.k
Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Chunya, walipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa uanzishwaji wa soko husika kwani biashara ya madini wilayani Chunya imekuwa ni ya uhakika huku wakineemeka na kulipa kodi mbalimbali Serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabishara wa madini wa Soko la Madini Chunya, Katibu wa Soko la Madini Chunya, Pius Madabuke alieleza kuwa uanzishwaji wa soko la madini umepelekea upatikanaji wa dhahabu wa uhakika kwani hapo awali wafanyabiashara wengi walikuwa wakitorosha madini hayo.
Alieleza kuwa manufaa mengine yaliyopatikana katika soko hilo ni pamoja na upatikanaji wa bei elekezi ambapo kwa sasa wanauza kwa faida kubwa hali iliyopelekea kufutika kwa masoko bubu yaliyokuwepo majumbani.
Katika hatua nyingine, Madabuke aliiomba Serikali kupitia Tume ya Madini kuongeza wataalam zaidi kwenye vituo vya kununulia madini na kuhamasisha Taasisi za Kifedha kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wa madini.
Naye Katibu wa Kituo cha Ununuzi wa Dhahabu Chunya, Emmanuel Nilla aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho wafanyabiashara wadogo wa madini wameondokana na dhana ya kuuzia madini ya dhahabu majumbani kutokana na faida kubwa inayopatikana kwenye uuzaji wa dhahabu kupitia katika kituo hicho.