Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi
akikabidhiwa hati ya msaada wenye thamani ya milioni 10 uliotolewa na Benki ya NMB PLC, kulia ni Meneja wa Benki hiyo Tawi la Kibaha Bw. Hosea Lyatuu.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Ukunga, Afya ya Uzazi Mama na Mtoto MNH-
Mloganzila Bi. Christina Mwandalima (kushoto) akiishukuru NMB kwa msaada
huo, katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. Mohamed Mohamed.
Bw. Hosea Lyatuu (wa pili kulia) akizungumza na uongozi wa Hospitali ya
Mloganzila wakati akikabidhi msaada kwa niaba ya Benki ya NMB.
Baadhi ya viongozi wa MNH-Mloganzila wakiwa katika picha ya pamoja na
wafanyakazi wa NMB mara baada ya kukabidhiwa msaada.
Vitanda 10, magodoro 10 na strecha mbili zilizokabidhiwa hospitalini hapa na
Benki ya NMB.
*********************************
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada kutoka Benki ya NMB
wenye thamani ya Tsh. Milioni 10 ambao unalenga kuunga mkono juhudi za
serikali za kuboresha huduma za afya nchini.
Akikabidhi msaada kwa niaba ya Benki ya NMB PLC, Meneja wa Benki hiyo tawi
la Kibaha, Bw. Hosea Lyatuu ametaja msaada huo ni vitanda 10, magodoro 10
pamoja na strecha mbili ambapo ameeleza kuwa NMB imekuwa ikitoa misaada
katika sekta tatu ikiwemo elimu na afya kwa lengo la kuisaidia jamii.
“Tumeamua kutoa msaada huu katika hospitali ya Mloganzila ili kuhakikisha kuwa kuna vitanda vya kutosha kwa ajili ya kutoa huduma za afya na benki yetu hufanya hivi ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii,” amesema Bw. Lyatuu.
Bw. Lyatuu amefafanua kuwa wanatambua mchango unaotolewa na watoa
huduma za afya hivyo wameamua kutoa msaada katika sekta hii ili kuhakikisha
jamii inapata huduma pasipo shida yoyote.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth
Magandi ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambao utaongeza idadi ya
vitanda vitakavyotumika kwa ajili ya kutolea huduma hospitalini hapa.
“Tunawashukuru kwa msaada huu kwani umekuja wakati muafaka wakati hospitali hii inajikia katika kuanzisha huduma mpya hivyo tunatumaini NMB mtaendelea na juhudi hizi kwani hospitali yetu bado inahitaji msaada wenu kwa lengo la kuhudumia jamii,” amesema Dkt. Magandi.