Ni sehemu Maarufu inayojulikana
kwa jina la Kijiji cha Wavuvi eneo la Kurasini wilayani Temeke ambapo kuna ufukwe mzuri wa bahari ambao
kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwa ni pamoja na uvuvi,
biashara ndogo ndogo na kutupia taka kutoka majumbani pamepelekea kuwa kero na kusababisha wakazi wa
Temeke na maeneo ya jirani kukosa eneo la kufurahi.
Kwa kuona umuhimu huo na shauku
ya kuwa na sehemu ya ufukwe Taasisi zisizo za kiserikali ikiwa ni pamoja na
TCCI, Mazingira Plus na Sanamare kwa kushirikiana na asasi nyingine zisizo
za kiserikali kama HUDEFO, ETE, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mazingira TV,
Ofisi ya Mtaa wa Kurasini, wakazi wa eneo la ufukwe na wadau mbalimbali
wameungana kwa pamoja kufanya usafi katika eneo hilo ili hapo baadaye lianze
kutumika kama sehemu ya watu kufurahi na kupumzika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wadau mbalimbali wa mazingira wamefurahishwa na hatua hiyo ya kusafisha eneo
hilo la fukwe na kuwaomba wavuvi, wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo
kuacha kutupa taka na kusema jukumu la kuweka safi eneo hilo sio lazima Serikali
ila wananchi pia wanaweza na kuhimiza kuwa eneo hilo panatakiwa kuwa na Choo ili
kuepuka magonjwa ya mlipuko kwa kuwa mpaka sasa watu wanaofanya shughuli
mbalimbali wanajisaidia vichakani.
Wakati huo huo ETE walishiriki katika kufanya usafi eneo hilo kwa lengo
la kuweka mazingira safi lakini pia kutumia Dijitali kuyasemea mazingira ambayo
hayawezi kujisemea yenyewe, kwa Hashtag #ETEMazingiraKidijidali kwa kutumia mitandao ya
kijamii na majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.