Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo akitoa salamu za serikali za pole kwa  wanafunzi na familia ambazo watoto wao wamepoteza maisha na kujeruhiwa kutokana radi katika kijiji cha Kindimbachini

Na Albano Midelo,Mbinga 

MKUU wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mheshimiwa Aziza Mangosongo ametoa majeneza matatu na kushiriki maziko ya wanafunzi watatu wa shule za Msingi Kindimba chini na Mapendo ambao wamepoteza maisha baada ya kupigwa na radi.

Mangosongo amewataja wanafunzi waliopoteza maisha baada ya kupigwa na radi kuwa ni Maria Hyera mwenye umri wa miaka kumi ,Alfons Hyera miaka minane Deus Kayombo miaka minane kutoka shule ya msingi Mapendano.

Mkuu wa Wilaya pia ametoa rambirambi  na kutoa pole kwa majeruhi 11 ambao wanaendelea kupata matibabu katika kituo cha  Afya Kindimbachini.

Ili kuhakikisha afya za majeruhi hao zinaimarika Mangosongo amemuagiza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kindimbachini kuhakikisha huduma za afya  zinatolewa bure.

Akitoa salamu za pole  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Andrew Mbunda amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa  huduma za afya  zitatolewa kwa ubora  kama alivyoagiza.

Naye  Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kindimbachini Dkt. Salum Bundala amesema katika tukio hilo  wanafunzi watatu wamepoteza maisha, na wanafunzi 20 walijeruhiwa na kufikishwa kituoni hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo kati yao 9 wameruhusiwa na 11 wanaendelea na matibabu na hali zao zinaimarika.

Akielezea tukio  hilo Mwalimu  Mkuu wa Shule ya msingi Mapendano Danstan Hyera  amebainisha  kuwa  majira ya saa tisa alasiri radi ilipiga na  wanafunzi 23 kati yao 20 walijeruhiwa  na wanafunzi  watatu walipoteza maisha.

 

Pichani wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo akiwafariji wanafunzi waliojeruhiwa baada ya kupigwa na radi katika kijiji cha Kindimbachini