Benki ya NMB imetangaza matokeo ya kiutendaji ya mwaka 2023, yakionesha kuvunja rekodi kwa mwaka mwingine tena baada ya kupata mafanikio ya kihistoria.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Januari 30, 2024 wakati akiwasilisha Taarifa ya Fedha ya Mwaka 2023, Afisa Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna amewashukuru wateja wa benki hiyo , wanahisa, wafanyakazi, washirika wote wa Benki, Serikali kupitia Benki Kuu na Watanzania wote kwa mchango wao thabiti na imani waliyonayo kwa Benki ya NMB.
Amesema benki imeongeza Jumla ya mapato ya Benki na kufikia Shilingi Trilioni 1.4 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 mwaka hadi mwaka.
Ameongeza kuwa uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato uliboreshwa zaidi hadi kufikia asilimia 39, wakati uwiano wa mikopo chechefu umeshuka hadi kufikia asilimia 3.2. Takwimu hizi zote ni chini ya ukomo wa kikanuni wa Benki Kuu wa asilimia 55 na asilimia 5 mtawalia.
Kutokana na ufanisi huu, Faida kabla ya Kodi imeongezeka kwa asilimia 26 hadi Shilingi Bilioni 775 huku Faida baada ya Kodi ikifika Shilingi Bilioni 542 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka. Hiki ni kiwango kikubwa cha faida na cha kihistoria kwa Benki ya NMB na sekta nzima ya fedha nchini.
Amefafanua kuwa Mizania ya Benki imeendelea kukua na kufikia jumla ya mali ya Shilingi Trilioni 12.2 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 19 kwa mwaka.
” Tuliendeleza ajenda ya ujumuishaji wa kifedha kwa kufungua akaunti mpya za wateja zaidi ya milioni 1.2, na kufanya jumla ya akaunti za wateja wetu kufikia zaidi ya akaunti milioni 7.1. Hii ni idadi kubwa zaidi ya wateja kwa taasisi moja ya fedha nchini, ” Amesema Ruth Zaipuna
Benki ya NMB iliwekeza zaidi ya Tsh. Bilioni 6 kwenye elimu, afya na mazingira, ikiwa ni sehemu ya dhamira benki hiyo kujitolea kusaidia jamii .