Kukamilika kwa kiwanda cha kuzalisha sukari Mkulazi kilichopo wilayni Kilosa mkoani Morogoro, kumetajwa kuwa kutawezesha kutoa ajira za moja kwa moja na za muda mfupi kwa vijana zaidi ya 5000.
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa bodi ya wadhamini mfuko wa hifadhi wa jamii (NSSF) Mwamini Juma Malemi alipokuwa katika ziara yake ya  kutembelea na kukagua kiwanda hicho ambacho hadi sasa kimekamilika kwa asilimia 100 na tayari kimeanza kazi ya uzalishaji wa sukari.
Aidha alisema kuwa sukari inayozalishwa katika kiwanda hicho itaanza kupatikana madukani hivi karibuni na pia kutakuwa na duka maalumu litakalouza sukari kwa bei elekezi ya kiwanda.
Kwa upande wake  mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Mkulazi  Dkt. Heridelita Msita alisema kuwa kiwanda hicho kimeanza kazi na amewahakikishia watanzania upatikanaji wa sukari ya kutosha kutoka kwenye kiwanda hicho.
Hata hivyo alisema  kuwa hadi sasa kuna baadhi ya makampuni yamekuwa yakiweka oda  kwaajili ya kupata sukari inayozalishwa  katika kiwanda hicho ambacho kimekuwa na manufaaa makubwa kwa wananchi na vijana kwa kupata ajira na kujiongezea kipato chao.
Ziara hiyo imefanyika  lengo likiwa ni kukagua na kujiridhisha namna kiwanda kinavyofanya kazi   ikiwemo mashamba ya miwa pamoja na mabwawa kwaajili ya umwagiliaji.