Na Neema Mbuja, Rufiji
Timu ya menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imetembelea mradi wa Bwawa la Julius Nyerere JNHPP huku ikieleza madhumuni ya ziara hiyo ikiwemo kufanya tathimini ya mwenendo wa ujenzi wa mradi unaokaribia asilimia 91 ifikapo Agosti mwishoni.
Lengo jingine la ziara hiyo ni kuangalia mwenendo wa ujenzi wa mradi na tathimini ya hali ya mvua za vuli zinazotarajiwa kunyesha kati ya Oktoba hadi Disemba kama ilivyotangazwa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA).Timu hiyo imeongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Tanesco Maharage Chande.
Akizungumza na waandishi wa habari, Chande amesema maendeleo ni mazuri hadi Julai tulifikia asilimia 90 na tunatarajia mwishoni mwa Agosti tutafikia asilimia 91 huku akiwapongeza wahandisi na wafanyakazi wa shirika hilo wanaosimamia mradi huo.
Amesema ukamilikaji wa mradi huu utatuwezesha kushinda mashindano haya kwa kuwa na umeme wa uhakika utakaokidhi mahitaji ya uchumi. Amesema timu ya menejimenti ya Tanesco imani kukamilika mradi huo utakuwa na mchango mkubwa wa kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme unaojitokeza katika miezi ya Oktoba na Desemba.
” Mambo yanakwenda na huenda upungufu wa umeme ukawa historia huko tunakokwenda, tutaongeza umakini katika utekelezaji wake,” amesema Maharage.
Kwa mujibu wa Chande kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya umeme hafi kufikia megawati 1,482.7 mwezi huu kutoka megawati 1,354 za mwaka 2022.
Ameifananisha hatua hiyo na mashindano makubwa ya kutumia umeme kutokana na mahitaji huku Tanesco ikiongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji kwa Watanzania.
Hali kadhalika pia Chande amesema timu ya menejimenti ya Tanesco imetembelea mradi huo kwa ajili ya kufanya tathimini kuhusu mvua zitakazonyesha miezi inayokuja.
” Endapo utabiri huo utakwenda kama ulivyopangwa basi bwawa hilo litajaa kwa haraka zaidi.Zikinyesha kama ilivyotarajiwa itakuwa heri, lakini zikiongezeka tumejiandaa kwa kuweka mipango itakayohakikisha kazi za mradi zinaendelea pasipo kupata changamoto,
Katika kuwaanda mapema wataalamu watakaoendesha mradi huo, Maharage amesema tayari wameshaongeza wafanyakazi zaidi ya 24 kwa ajili ya kujiandaa kuendesha mchakato huo utakapokamilika.
Amefafanua kuwa ili mradi huo uanze kufanya kazi unahitaji wafanyakazi 221 watakaouendesha pindi utakaokamilika, akisema kwa sasa jumla wapo zaidi ya 90 na watakuwa na wakiwapeleka kwa awamu kulingana na mradi utakapofikia.
Chande amesema jumla watumishi 221 wanahitajika kuendesha mradi huo, lakini hawatapelekwa kwa wakati mmoja, bali kwa makundi yatakayoenda kwa wakati husika
.Amesema kundi lililopo sasa hivi linahusika na utalaamu wa uhandisi mitambo ya umeme.
“Kutakuwa na wafanyakazi madaktari, walimu wa shule za awali, wahasibu. Tutaendelea kuongeza wafanyakazi kwa makundi kulingana na hatua ya ujenzi wa mradi utakapofikia,
Mkurugenzi wa Fedha wa shirika hilo, Renatha Ndege amesema menejimenti ya shirika hilo imeamua kutembelea mradi huo ili kuangalia mwenendo wa utekelezaji wake, akisema ukikamilika Juni mwakani utakuwa mkombozi mkubwa kwa Watanzania.