Na Sophia Kingimali
Wizara ya Madini imeendelea kupokea Maoni ya Wadau wa sekta hiyo kuhusu mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria na baadhi ya Kanuni zitakazosimamia shughuli za Sekta ya Madini.
Akiongoza Kikao Kazi kinachoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt. Suleiman Serera amewataka wadau wa Sekta ya Madini kuchangia mawazo yao kwa uhuru ili kuboresha na kuongeza ufanisi katika shughuli za sekta hiyo.
Aidha, Dkt. Serera ameyataja maeneo yatakayopokelewa mapendekezo yake na kujadiliwa leo ni pamoja na Kanuni ya Madini Ushiriki wa Serikali za Mwaka 2022, Kanuni ya Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2022, Kanuni ya Haki Madini za Mwaka 2018, Kanuni ya Masoko ya Madini za Mwaka 2019 pamoja na Kanuni za Uongezaji Thamani Madini za Mwaka 2020.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi upande wa Mazingira, Mhandisi Ally Samaje amezitolea ufafanuzi Kanuni mbalimbali zinazopendekezwa ambapo amesema kuna baadhi ya Kanuni zina changamoto katika utekelezaji wake ambapo suluhisho lake ni kuzifanyia Marekebisho.