Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo, Kilimanjaro
SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo
inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Nchini
(TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.
Kwa kuzingatia hatua hizo, Wizara ya
Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha
kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga
(Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 21 Octoba 2019 wakati akizungumza kwenye
ufunguzi wa Programu ya kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani pamoja na
uzalishaji bora wa mazao ya viungo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Hotel ya Uhuru Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Mhe Hasunga ameyataja maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji wa haraka. Mosi, Utekelezaji wa adhma ya serikali
kuendeleza kilimo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya
Pili (ASDP II) kwa kusimamia thabiti nguzo ya programu hiyo
ikiwemo Usimamizi endelevu wa matumizi ya maji na ardhi.
Alisema kuwa Lengo la ASDP II ni kuleta
mageuzi katika Sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija, kilimo
cha kibiashara, kuongeza pato kwa wakulima hivyo nilazima kuwekwa mkakati
madhubuti wa utekelezaji ili kufikia nalengo yaliyokusudiwa.
Vilevile, alisema kuwa serikali
imekusudia Kuboresha mazingira wezeshi, uratibu, ufatiliaji na tathmini katika
sekta ya kilimo hivyo wataalamu katika Wizara ya kilimo wanapaswa kuongeza kasi
ya uwajibikaji ili kutimizi adhma hiyo.
Alisema Wizara ya kilimo itaweka
mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa bei ya Mazao inaimarika huku akisisitiza
kuwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atahakikisha
wakulima wanapata masoko ya mazao yao.
Amesema kuwa Wizara ya Kilimo imetayarisha Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya kuvunwa.
Alisema kuwa mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na malengo endelevu ya Dunia ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama wa chakula na lishe na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa Mataifa kati ya Malengo 17.
Mkakati huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha, Mkakati huo umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.