Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utalii ya Camp Bastian Mikumi ,Gabriel Mwakalukwa  akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha. Kampuni ya utalii  ya  Camp Bastian Co.Ltd iliyopo Mikumi  inayohusika na malazi pamoja  na uandaaji wa safari za wageni wa ndani  na nje kutembelea vivutio vinavyopatikana Tanzania imefanikiwa kupata tuzo nane mfululizo kutokana na huduma nzuri wanazotoa kwa watalii.
Aidha katika tuzo hizo mbili zimetolewa  na TANAPA huku sita zikitolewa na Trip Advisor  ambapo kampuni hiyo imeshinda tuzo hizo kwa ukanda wa kusini  Magharibi  mwa Tanzania .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni hiyo ,Gabriel Mwakalukwa amesema kuwa,kampuni hiyo imepata tuzo hizo kwa miaka sita mfululizo kati ya Camp za watalii 60 zilizoko  katika ukanda huo. 
Amesema kuwa,wamekuwa wakitoa huduma nzuri kwa watalii kutokana na mafunzo bora  ambayo wamekuwa wakifundisha wafanyakazi wake kuweza kuwahudumia  watalii na kufurahia  huduma inayotolewa  na kampuni hiyo. 
“Kutokana na kupata tuzo hizo tumeweza kujifunza mambo mengi sana katika kuhakikisha tunaboresha huduma zetu pamoja na kuhakikisha tunatimiza ahadi  yetu ya kuwahudumia watalii ipasavyo na kuhakikisha tunaendelea  kuzipambania  tuzo hizo badala  ya kubweteka  .”amesema  Mwakalukwa.
Aidha amesema kuwa kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua filamu  ya Royal Tour kimeleta mafanikio  na mabadiliko makubwa ikiwemo kuongeza idadi  kubwa ya watalii  wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.
Mwakalukwa amesema kuwa,TANAPA imeangalia sana sekta ya  utalii kusini kwani ilishasahaulika  sana ila kwa sasa wametupia jicho kwa karibu sana hali ambayo imefanya biashara hiyo kuchangamka  katika ukanda huo.
“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa namna ambayo anazidi kuipa kipaumbele sekta ya utalii hapa nchini jambo ambalo linatoa fursa kwa watalii wengi kutembelea hapa nchini na kuweza kuongeza fedha za kigeni.”amesema .