Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa ya tukio la ajali ya
jiwe kuanguka na kusababisha kifo na majeruhi kwa wanafunzi wa Shule
ya Secondary Mwinuka iliyopo Kata ya Kitangili, Wilayani Ilemela.
Tukio hilo limetokea tarehe 17.03.2023 muda wa saa 07:00 asubuhi katika
eneo la shule ya Sekondari Mwinuka, ambapo wanafunzi walikuwa
wanatekeleza adhabu waliyopewa na Mkuu wa Shule hiyo baada ya
kukamatwa wanaongea lugha ya Kiswahili kinyume na taratibu za shule
hiyo ambapo wanatakiwa kuzungumza lugha ya kingereza wawapo
shuleni.
Baada ya kupewa adhabu hiyo iliyotolewa jana tarehe 16.03.2023 na Mkuu
wa Shule, baadhi ya wanafunzi walitekeleza adhabu hiyo ambapo
waliambiwa kuchimba kifusi na kujaza sehemu zenye mabonde, lakini
Glory Faustine na Emmanuel Lyatul hawakukamilisha adhabu hiyo na
ilipofika asubuhi ya leo walifika shuleni hapo kwa ajili ya kukamilisha
adhabu.
Wakiwa ndani ya shimo lenye kifusi ghafla waliangukiwa na jiwe kubwa
lililokuwa juu ya shimo hilo na kusababisha kifo kwa mwanafunzi aitwaye
Glory Faustine Feliciani, Miaka 14, Mwanafunzi wa Kidato cha
Kwanza, Mkazi wa Kirumba, na majeruhi kwa Emmanuel Lyatul
Michael, Mika 13, Mwanafunzi Kidato cha Kwanza, Mkazi wa Ibanda
Busisi, ambaye amevunjika mguu wa kulia.
Jeshi la Polisi linamshikilia Mwalimu Mkuu wa shule ya Secondary
Mwinuka aitwaye Mwalu Steven, Miaka 51,Mwalimu Mkuu, Mkazi wa
Buhongwa pamoja na mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo aitwaye
Theonest Malosha, Miaka 35,Mwalimu na Mkazi wa Kahama Buswelu
kwa mahojiano Zaidi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya
Mkoa Sekou Toure na utakabidhiwa kwa ndugu baada ya uchunguzi na
hali ya majeruhi inaendelea vizuri.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi na wazazi kuendelea kuwa na
subra katika kipindi hiki ambapo linafanya kila namna kuhakikisha
linachukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika aidha kwa uzembe au
kwa kutotimiza wajibu wake ipasavyo.