Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 15,2023 katika Ofisi za LHRC Jijini Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Sheikh Ponda Issa Ponda akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 15,2023 katika Ofisi za LHRC Jijini Dar es Salaam.
*************************
NA MWANDISHI WETU
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kimeishauri Tume ya Haki Jinai inayoendelea na zoezi la ukusanyaji maoni nchini kutumia fursa hiyo kutoa mapendekezo kwa Rais juu ya watuhumiwa wote wa makosa ya ugaidi waliokaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kesi kusikilizwa ili Mkurugenzi wa mashtaka DPP kuwaachia huru.
Ushauri huo wa LHRC kwa kushirikiana na Jumuiya na taasisi za Kiislam umekuja mara baada ya taarifa ya kifo cha Sheikh Saidi Mohammed Ulatule kilichotokea Machi 4 mwaka huu aliyekuwa akituhumiwa kwa ugaidi ambapo aliwekwa gerezani tangu mwaka 2016.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 15,2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC Anna Henga ameshauri mwendesha mashtaka wa serikali awafutie mashtaka au awafikishe mahakamani kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Sheikh Ponda Issa Ponda pamoja na mmoja wa Familia ya marehemu Ulatule wameiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria za vyombo vya dola pamoja na kutoa haki kwa mahabusu waliokaa muda mrefu gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 10 mwaka huu na Mkuu wa Magereza Dar es Salaam, George Wambura alisema kifo cha sheikh huyo kilichotokea Machi 4, mwaka huu, kimetokana na ugonjwa wa shinikizo la moyo uliokuwa unamkabili tangu mwaka 2017 alipoingia gerezani.