Katibu Tawala mkoa wa Arusha ,Missaile Musa akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo.
**********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa amewataka wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Arusha kubaini makundi au vikundi yanayojihusisha na uzalishaji wa bidhaa zao, ili kupata mafunzo kutoka Tume ya Ushindani (FCC), kwa lengo la kuongeza tija kwa bidhaa na viwango kwenye ushindani wa soko.
Mussa ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wa masuala ya ushindani na udhibiti wa bidhaa bandia kwa wazalishaji na wamiliki wa viwanda Kanda ya Kaskazini.
Amesema endapo vikundi vinavyopewa mikopo na halmashauri vikipata mafunzo ya udhibiti wa ushindani wa kibiashara, vitawezesha bidhaa zao kuingia katika masoko kutokana na ubora.
“Nataka mzingatie kwa makini mafunzo haya ili kunusuru masoko ili yabaki salama na ya ushindani na watumiaji wa bidhaa hizo pia wawe salama pasipo kuwa na athari ili vikundi vinavyopewa mikopo na halmashauri vikipata mafunzo haya ya udhibiti na ushindani wa kibiashara itawezesha bidhaa zao kuingia katika masoko makubwa kutokana na ubora wa bidhaa zao”. amesema Mussa.
Aidha Mussa amesema lengo la mafunzo hayo kwa wakurugenzi ni kuweza kuwasaidia wazalishaji kukuza biashara pamoja mnyororo wa thamani ikiwemo udhibiti wa bidhaa bandia na ukaguzi kwa walaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.
Mussa amewapongeza FCC na kuwataka waendelee kwa kasi zaidi ili waweze kulisaidia Taifa kutokuwepo na bidhaa bandia zinazo lighalimu Taifa hasa katika ukuaji wa kiuchumi kwa wazalishaji
“FCC mnao umuhimu mkubwa sana katika jamii na hasa katika kuliendeleza Taifa letu kiuchumi, Rai yangu kwa Taasisi na mashirika mengine kutafita namna nzuri ya kuendelea kujifunza katika ustawi wa uzalishaji wa bidhaa na upanuzi wa biashara nchini kwa kuendelea kuwafuata FCC kwa kila jambo ili iwasaidie”. amesema Mussa.
Kwa upande wake Mkuu wa FCC Kanda ya Kaskazini, Nonge Juma aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa FCC, amesema mafunzo hayo kwa wafanyabiashara wa viwanda vidogo vya kati na vikubwa yanalengo la kuwezesha kuleta tija katika ushindani wa biashara wanazozalisha ikiwemo kudhibiti bidhaa bandia zisizizosajiliwa na kuleta athari kiuchumi.
Juma amewataka wafanyabiashara hao na wenye viwanda vya uzalishaji kuhakikisha wanazongatia maadili ya biashara ili kuhakikisha soko linabaki shindani kwa manufaa ya kumlinda mtumiaji
“Ongezeko la bidhaa bandia linaporomoko la kiuchumi viwandani kwa kuliona hilo tumeona ni bora kuwapa elimu hii wazalishaji wa biwandani ili kuweza kuona namna bora ya kulinda bidhaa zao pamoja na mlaji”. amesema Juma.
Aidha amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kutekeleza sheria inayo wataka kutoa mafunzo mbali mbali ili kuendeleza ujuzi kwa wazalishaji ambapo pia hadi hivi sasa wameshatoa mafunzo hayo Zanzibar kwa kuongeza uwelewa kwa wazalishaji.