*********************

NA  VICTOR MAKINDA

Katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, kuepukana na magonjwa mbali mbali ya mlipuko,  Mamlaka  ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Igunga ( IGUWASA) wilayani Igunga Mkoani  Tabora ipo katika hatua za mwisho za kuanza kuteleza mradi wa ujenzi  wa mfumo wa kusafisha  maji taka utakaogharimu Shilingi Bilioni 1.8.

Hayo yameelezwa na  Mkurugenzi wa IGUWASA, Humphrey Mwiyombela,  wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Igunga jana  kueleza hatua mbali mbali za miradi inayotekelezwa na mamlaka hiyo pamoja na mipango ya baadae ya kuendelea kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira wilayani hapa.  

Mwiyombela alisema kuwa Mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuanza kwa mradi huo  ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuufanya mji wa Igunga kuwa wa kisasa zaidi kwani ujenzi huo utakwenda sambamba na ununuzi wa magari mawili ya maji taka.

“ Kwa sasa hatuna eneo rasmi  lililoandaliwa kitaalamu kwa ajili ya kutumika  kumwaga maji taka hali ambayo inahatarisha afya za wananchi. Alisema Mwiyombela..

Akizungumzia upatikanaji wa maji safi wilayani  Igunga, Mwiyombela alisema kuwa IGUWASA imefikia asilimia 89 ya kusambaza huduma ya maji kwa  wananchi ikiwa malengo ni kufikia  matakwa ya  ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka  2020-2025 inayoagiza upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 ifikapo mwaka  2025.

“ Katika kuhakikisha tunaongeza idadi  ya watumiaji wa maji tunaende kuweka magaea kusambaza mtandao wa maji maeneo mbali mbali sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia  maji safi kwa afya zao  ili waweze kutumia maji safi na kuachana na maji ya madimbwi.” Alisema.

Aliongeza kusema kuwa katika kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia maji safi kwa kuunganishiwa mabomba,  IGUWASA huwaunganishia huduma hiyo kwa mkopo ambapo hutakiwa kulipa kidogo kidogo baada ya malipo ya awali.