Angeline Mabula akishuhudia mkurugenzi wa NHC Nehemia Mchechu akitia Saini katika makubaliano ya shirika hilo na Bank ya Absa Tanzania, jana tarehe 17 February 2023.
Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Angeline mabula akiteta jambo na mkurugenzi wa NHC pamoja na mkurugenzi wa Absa Tanzania ndugu Abdi Mohammed jana katika utiaji saini wa makubaliano kati ya NHC na Absa Tanzania.
…………………………
NA MWANDISHI WETU
Shirika la Nyumba la Taifa(NHC)Limeingia mkataba wa makubaliano na benki ya Absa Tanzania wenye lengo la kuwawezesha watanzania kupata mikopo ya nyumba za Shirika hilo.
Akizungumza katika hafla ya utilianaji Saini wa mkataba huo iliyofanyika kwenye eneo ulipo mradi mkubwa wa nyumba za Shirika hilo Morocco Square Jijini Dar es salaam, waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amepongeza hatua hiyo na kusema kuwa itakuwa ni manufaa makubwa Kwa wateja wa benki ya Absa, Shirika la nyumba la Taifa pamoja na wanunuzi wa nyumba hizo.
Waziri Dkt Mabula amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya nyumba unahitaji kiwango kikubwa Cha fedha hivyo benki na taasisi za fedha Zina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya nyumba nchini hivyo makubaliano kati ya Benki ya Absa Tanzania na NHC yatakuwa chachu kubwa ya kuwawezesha watanzania kumiliki nyumba Kwa njia za mikopo.
“uwekezaji katika sekta ya nyumba umechangia Kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa ajira, mitaji, kipato, akiba na kuimarisha afya na elimu, serikali zote duniani zinaheshimu mchango wa sekta za nyumba katika kukuza uchumi na ni kichocheo kikubwa Cha kudumisha amani, hivyo ni dhahiri kwamba hakuna nchi inayoendelea duniani bila kutoa kipaumbele Kwa sekta ya nyumba”amesema Dkt Mabula
Dkt. Mabula aliongeza kuwa nia ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuona serikali na sekta binafsi zinashirikiana katika kuondoa changamoto ya uhaba wa nyumba kwa watanzania wote kwa kuhakikisha wanakuwa na nyumba za kisasa watanzania wanakuwa na nyumba bora hivyo mpango huo wa Absa na NHC utatoa fursa za wananchi kupata mikopo ya nyumba.
Aidha ametoa wito kwa benki na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo ya nyumba hapa nchini kutafuta mbinu za kuwezesha mikopo hiyo iwe na riba nafuu ili hata wananchi wenye kipato cha chini waweze kumudu gharama hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa,NHC Nehemia Mchechu amesema shirika hilo litashirikiana vyema na benki ya Absa katika utoaji wa nyumba za kisasa kwa wateja watakaokopa nyumba hizo kupitia benki hiyo.
Aidha aliongeza kuwa pia shirika hilo pia kutawajengea nyumba wateja wake ambao walinununua viwanja vyao kwenye shirika hasa miradi ya Safari City iliyopo Arusha mara baada ya wateja hao kupata mikopo ya ujenzi wa nyumba kupitia Absa.
Hata hivyo Bw Mchechu ameongeza kuwa mraadi wa Samia Housing Scheme utatekelezwa nchi nzima na wameanza na eneo la Kawe jijini Dar es Salaam ambapo asilimia 70 ya mradi huo imepata wateja.
Aliongeza kuwa shirika hilo lina mpango wa kuifanya Kawe kuwa mji wa kisasa ambao utaendesha shughuli zake kwa saa 24 na hata eneo kubwa la michezo hapa nchini (Sports Arena)itaanza kujengwa eneo la Kawe.
Mchechu ameongeza kuwa kupitia ushirikiano wa kibiashara kati ya benki ya Absa na shirika hilo sasa wateja wa NHC hawapaswi kuwa na hofu kwani watapata mikopo yenye riba nafuu ambayo itawawezesha kununua nyumba za shirika hilo huku akitoa wito kwa watanzania waishio nje ya nchi (diaspora)kutokuwa na shaka ya kupata nyumba za shirika hilo kupitia benki hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania amesema kuwa baada ya benki hiyo kufanya tafiti wamegundua kuwa watanzania wamekuwa wakihangaika kupata mikopo kwa ajili ya kununua au kujenga nyumba za kisasa hivyo kupitia mkataba huo sasa baina ya Absa na NHC watanzania wataweza kumiliki nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa benki hiyo pia iligundua haijawafikia wateja wake wengi wakiwemo Diaspora na watu walioajiriwa hivyo wakaamua kuja na mikopo hiyo ambapo mteja anaweza kukopa mpaka shilingi bilioni 1
Aidha ameushukuru uongozi wa shirika la nyumba la Taifa kupitia mkurugenzi wake kwa kuingia mkataba wa makubaliano hayo ambao utakuwa chachu ya kutimiza ndoto za watanzania wengi za kumiliki nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.