WAZIRI wa Ardhi Nyumba an Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 7,2023 jijini Dodoma kuhusu ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya sekta ya ardhi mkoani Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Ardhi Nyumba an Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula,amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza kipindi cha msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi hadi April 2023.
Hayo ameyasema leo Februari 7,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya sekta ya ardhi mkoani Dodoma.
Dkt. Mabula amesema kuwa Wizara yake imejipanga kuwahudumia kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata nafuu ya msamaha wa riba ya kodi ya pago la ardhi iliyotolewa na Mhe Dkt. Samia .
‘’Wajulisheni wananchi kuwa Mhe Rais Samia ameongeza muda wa msamaha wa riba ya malimbikizo na Wizara imejipanga kikamilifu ili kuwezesha wananchi kupata nafuu ya msamaha wa riba ya kodi ya pango la ardhi iliyotolewa’’ amesema Dkt Mabula.
Hata hivyo Waziri Mabula amesisitiza kuwa wananchi, mashirika na kampuni ambazo hazitatumia fursa hiyo Wizara imejipanga kuchukuwa hatua za kisheria kukusanya kodi pamoja na malimbikizo.
“Hivyo, Natoa rai kwa taasisi na mashirika ya umma na wananchi wote kutumia muda uliotolewa hadi April 30 na Mhe. Rais kunufaika na msamaha wa riba uliotolewa na Serikali kulipa deni la msingi (principal amount) ili wasamehewe riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi” amesisitiza Dk. Mabula
Aidha Waziri Mabula amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2022, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 90.9 sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 121.
“Makusanyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yameongezeka kwa Shilingi bilioni 33.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka wa Fedha 2021/22” Amesema Dk.Mabula
Dkt Mabula amesema kuwa wananchi 6,211 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo sawa na shilingi 11,931,537,409.80.
“Serikali inaamini kuwa fedha hizo zilizosamehewa zimeenda kuleta nafuu kwa wahusika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini” ameeleza
Waziri Mabula amemshukuru Mhe.Rais, Dkt Samia Suluhu Hassani kwa uamuzi wake wa kusamehe kiasi kikubwa hicho kwa lengo la kuwaondolea mzigo wa madeni wananchi na taasisi mbalimbali.
Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi ambapo wananchi walio na malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia Julai hadi Disemba, 2022.
Hata hivyo ameelekeza ofisi zote za ardhi nchini kutoa huduma siku zote hadi mwisho wa mwezi April 2023 ili kuwezesha upatikanaji huduma za ukadiriaji kodi kwa wakati na kuwasihi wananchi kuendelea kutumia njia za kielektroniki alizozieleza kuwa zimeanza kutolewa na benki washirika za CRDB na NMB katika kukadiria kulipa kodi.