Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amezindua rasmi Matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kuitumia kufanikisha mikutano.
Kupitia njia hiyo Taasisi zote chini ya Wizara ya Maji zitakuwa na uwezo wa kufanya mikutano na kuwasiliana Kwa wakati mmoja.
Uzinduzi huo ameufanya leo Februari 3, 2023 akiwa ofisi za Idara ya Rasilimali za Maji Jijini Dodoma katika kikao ambacho kiliwahusisha Menejimenti ya Wizara iliyokuwa katika ofisi za Wizara, Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni Taasisi zote za Wizara ambazo ziliunganishwa kutokea maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mhe Waziri ametoa kongole kwa kitengo cha TEHAMA na Watehama wa Wizara kwa kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo na kuwataka wadau wa sekta ya maji kote nchini kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo kufanikisha lengo la wizara la kuwafikishia Watanzania huduma ya majisafi na salama.
Aidha, Waziri Aweso Amesema Mhe. Rais ameonesha nia ya dhati ya kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya maji hivyo watumishi wa wizara wanapaswa kuonesha mfano.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatapunguza gharama na muda kwani kuanzia sasa watumishi hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya vikao.