Kaimu Meneja wa Mkoa wa Kodi wa Ilala, Bw. Steven Kuzeni akieleza taarifa ya utekelezaji wa Ofisi yake kwa Mhe. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alipotembelea Ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishina (Operesheni) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Albert Kingu akimkabidhi Mhe. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ‘Road map’ na makubaliano ya malengo waliyojiwekea Mamlaka hiyo na Mameneja wa Mikoa katika kuhakikisha wanafikia malengo ya ukusanyaji mapato katika Mikoa yao.
*******************************
Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka mifumo imara ambayo itamtambua kila mfanyabiashara na bidhaa anayouza ili kuweza kukusanya kodi stahiki na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.
Mhe. Kijaji aliyasema hayo kwa viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa Mikoa ya Kodi ya Ilala na Kariakoo, wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Mamlaka hiyo inayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba inavuka lengo la makusanyo iliyojiwekea ili kuweza kumsaidia Mhe. Rais DKt. John Pombe Magufuli, atekeleze majukumu yake kwa ufanisi na kulifikisha Taifa pale alipodhamiria.
“Naiagiza Mamlaka kuanza zoezi la kukagua watumiaji wote wa mashine za utoaji risiti za kieletroniki (EFD) hasa kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti na kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza makusanyo na kupelekea Taifa letu kujiendesha kupitia fedha zetu wenyewe kwa kuwa hakuna Taifa huru bila mapato’’ alisisitiza Dkt. Kijaji
Aliwataka Maafisa wa TRA kutokaa ofisini badala yake wawatembelea wafanyabiashara ili kuhakiki matumizi ya mashine za utoaji wa risiti za kieletroniki (EFD).
Awali Meneja wa Ofisi ya Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Bw. Alex Katundu alimueleza Mhe. Kijaji kuwa Mkoa wake wa kikodi una jumla ya wafanyabiashara waliosajiliwa na Mamlaka hiyo 22,279 na kati ya hao wafanyabiashara 16,068 wanatumia mashine za EFD.
Alisema Mkoa wa kodi wa Kariakoo kwa mwaka 2018/19 walidhamiria kukusanya shilingi bilioni 138.66 lakini walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 109 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya malengo waliyojiwekea.
Katika Mkoa wa kikodi wa Ilala, Kaimu Meneja Bw. Steven Kuzeni amesema katika kuhakikisha Mkoa wake unakusanya ipasavyo kodi ya Majengo, wamedhamiria kusajili majengo yote yanayozunguka Mkoa huo wa kikodi na hadi sasa wameshasajili majengo katika kata 26 kati ya kata 32 zilizopo katika eneo lake.
“Ofisi yangu kwa mwaka 2019/20 ina mkakati kabambe wa kuhakikisha inaongeza idadi ya walipa kodi ya mapato na wale wa ongezeko la thamani (VAT)” Aliongeza Bw. Kuzeni.
Katika hatua nyingine Kijaji amewapongeza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwezi Septemba ambapo imekusanya sh. trilioni 1.76, kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa tangu nchi ipate uhuru na kuwahimiza kukaa pamoja na Taasisi zote zinazofanya kazi kwa karibu na Mamlaka hiyo ili kuona ni kipi kinaweza kuboreshwa zaidi ili kuwapa fursa Watanzania kulipa kodi bila Serikali kuwalazimisha.