Afisa muuguzi ambaye ni Mratibu wa maswala ya ukatili wa kijinsia kutoka hospitali ya Mount Meru ,Lilian Lukumay akizungumza na watoto  waishio  mazingira  hatarishi  kuhusu maswala ya ukatili wa kijinsia. 
Mwenyekiti wa taasisi ya Vijana kwa pamoja tunaweza(VIPATU) ,Jane Edward akizungumza kuhusiana na semina hiyo ya maswala ya ukatili wa kijinsia 
Baadhi ya watoto hao  wakipatiwa semina hiyo jijini  Arusha 
***********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha .Wazazi pamoja na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wa kiume pamoja na kuzungumza  nao kuhusiana na maswala ya ukatili wa kijinsia kwani  wao ndio wanaoongoza kufanyiwa vitendo hivyo. 
Aidha wazazi wengi wamekuwa karibu sana na watoto wa kike na kuwasahau  watoto  wa kiume na hivyo kujikuta  wao ndio waathirika zaidi wa vitendo hivyo kutokana na kutokuwa na elimu yoyote. 
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Afisa muuguzi  ambaye pia ni Mratibu wa maswala ya ukatili wa kijinsia kutoka hospitali ya Mount Meru,Lilian Lukumay  wakati akizungumza  na watoto wanaotoka kwenye mazingira hatarishi wanaolelewa  katika vituo mbalimbali ambapo waliweza kupatiwa elimu juu ya maswala ya ukatili wa  kijinsia semina  iliyoandaliwa na taasisi ya Vijana kwa pamoja tunaweza(VIPATU).
Amesema kuwa, elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa watoto  wa kiume kwani ndio waathirika wakubwa wanaofanyiwa vitendo  vya ukatili na hii imekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali.
“Tunaomba sana wazazi na walezi mkae  chini na watoto wenu  wa  kiume waelezeni swala la ukatili wa  kijinsia bila kuwaonea  aibu yoyote kwani  zamani elimu hiyo ilikuwa ikilenga  zaidi kwa watoto  wa kike ila kwa sasa hivi hali  ni mbaya sana pande zote pindi zimetakiwa kupewa elimu ili wafahamu na kujua  madhara  take na hatua za kuchukua  pindi wanapofanyia  vitendo hivyo “amesema .
Aidha ameongeza kuwa,takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watoto wanafanyiwa  vitendo vya ukatili  majumbani  huku asilimia 40 wakifanyiwa mashuleni  huku  ukatili wa  kingono  ukiongoza zaidi  kwa watoto  hao. 
Mwenyekiti wa  Taasisi ya VIPATU ,Jane Edward alisema kuwa, lengo  kubwa la kuandaa semina hiyo ni  kuwakutanisha watoto hao na kuweza kupata  elimu juu ya maswala la ukatili wa kijinsia kwani wengi wao hawana elimu  juu ya maswala hayo .
“Tumeamua  kuwakutanisha hawa watoto  wanaolelewa kwenye vituo mbalimbali pamoja na wale wanaoishi  mitaani  ili waweze kupata elimu kuhusu maswala hayo  kwani  wengi wao wamekuwa wakifanyiwa  ukatili  wa kingono na kukosa sehemu ya kuripoti  matukio  hayo ,hivyo  kupitia elimu hii itawasaidia  sana kuchukua  tahadhari mapema na kuweza kuwasaidia  wenzao  kwa ujumla.”amesema Jane.
Jane amesema kuwa, ukatili wa kijinsia unaendelea kushika kasi kwa watoto ambapo wanaofanyiwa zaidi  ni wanaume ,hivyo kuyataka mashirika mbalimbali pamoja na wadau kuongeza  nguvu  katika kusaidia watoto  hao  ili  waweze kuondokana  na changamoto  mbalimbali  ikiwemo za ukatili wanaofanyiwa majumbani na mashuleni.
Baadhi ya walezi wa  vituo hivyo,Anna Ismali kutoka kituo cha Grace na Dorcas  kutoka kituo cha Moshono  wamesema kuwa,wanashukuru sana Taasisi hiyo kwa namna ambavyo imewawezesha kufanyika kwa semina hiyo kwani watoto wengi hawana uelewa  wa  kutosha juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia ,huku wakiomba wadau mbalimbali kufika  vituoni na kutoa elimu hiyo ili watoto  hao waweze kunufaika na kuokoa  kizazi cha  kesho.