Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF wa Kikundi cha Twiyendage kilichopo Wilaya ya Ubungo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini Dar es salaam.
Sehemu ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Hapa Kazi tu na Umoja Group vya Wilaya ya Kigamboni wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Sehemu ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Jiwezeshe Women Group Wilaya ya Temeke wakionesha baadhi ya bidhaa wanazotengeneza, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TASAF, Bi. Salome Mwakigomba akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi jijini Dar es Salaam, iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
……………………………..
Na. Veronica Mwafisi – Dar es salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo walengwa wa TASAF walio kwenye vikundi, kupitia fedha za asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili mikopo hiyo iboreshe maisha ya kaya maskini nchini kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia.
Mhe. Ndejembi ametoa rai hiyo, kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Ndejembi amesema, ameweza kutembelea vikundi mbalimbali vya walengwa wa TASAF katika Halmashauri zote zilizopo jijini Dar es salaam na kuona utekelezaji wa kazi za vikundi mbalimbali vinavyojumuisha Vijana, Wazee, Walemavu na Wanawake.
“Wilayani Kinondoni kuna vijana walio kwenye vikundi vya TASAF walipatiwa mikopo wa pikipiki ambapo wamemudu kurejesha, pia wanawake Temeke walio kwenye vikundi vya TASAF wamepatiwa mikopo ya shilingi milioni 10 na Ilala wamepatiwa milioni 30 ambayo imewawezesha kuboresha maisha yao na kujishughulisha na ujasiliamali,”Mhe. Ndejembi amefafanua.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bi. Salome Mwakigomba amesema TASAF imefanya jitihada kubwakuhamasisha uundaji wavikundi vya walengwa katika halmashauri zote ambazo Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unatekelezwa hivyo wakipatiwa mikopo hiyo ya asilimia 10 watendelea kuboresha maisha yao.
Bi. Mwakigomba amesema, TASAF itatekeleza maelekezo ya Ndejembi ya kuwahamasisha walengwa wa TASAF kuwa na miradi endelevu ili wajiongezee kipato kitakachowawezesha kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).